0


FEDHA zilizotengwa na Rais John Magufuli kwa ajili ya kugharimia elimu ya bure nchini, zimeanza kutafunwa baada ya kubaini kuwapo kwa udanganyifu unaofanywa na walimu wakuu kwa kuongeza idadi ya wanafunzi hewa ili kupata fedha zaidi.

Kutokana na hali hiyo, wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam na Manispaa ya Arusha, zimebaini udanganyifu huo na kuchukua hatua za awali kwa kusimamisha walimu wakuu wa shule husika na pia kuziagiza mamlaka husika kuwavua uongozi walimu hao.

Hivi karibuni, Rais Magufuli aliwaagiza wakuu wa wilaya zote, kushughulikia udanganyifu unaofanywa na walimu wakuu wanaotafuna fedha kwa kuweka wanafunzi hewa katika suala la elimu bure baada ya serikali kuanza kutoa elimu bure Januari mwaka huu, ikitenga Sh bilioni 18.7 kila mwezi.

Wanafunzi hewa Kinondoni
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi aliwaambia waandishi wa habari jana Dar es Salaam kuwa kubainika kwa wanafunzi hao kumekuja baada ya kuagiza mkurugenzi na watendaji kufanya uhakiki shule kwa shule ili kubaini wanafunzi hewa, waliowekwa na walimu wakuu wasiokuwa na uzalendo na kujipatia fedha kinyume cha sheria.

“Hadi kufikia leo (jana) tumebaini wanafunzi hewa 3,462 kutoka shule 68 za msingi na wanafunzi 2,534 kutoka shule 22 za sekondari ambao wameingizwa, ni jambo la kusikitisha fedha za serikali zinapotea kwa sababu ya walimu wakuu wasio waaminifu,” alisema Hapi.

Alizitaja baadhi ya shule za msingi zilizokutwa na wanafunzi hewa ni Msisiri B, Msewe, Golani, Kibangu, Kimara Baruti, Ubungo Kisiwani, Shekilango, Tandale, Makoka, Mbezi Luis, Kijitonyama, Kinondoni, Mburahati, Makumbusho, Makongo, Kawe A na Ubungo Plaza.

Shule za sekondari ni Boko, Bunju A, Kambangwa, Kawe Ukwamani, Kigogo, Kiluvya, Mbweni, Matosa, Maramba Mawili, Mburahati, Salma Kikwete, Saranga, Temboni, Mabibo, Makoka, Luguruni na Mtakuja.

Hapi alisema baada ya kubainika mambo yote hayo, hatua mbalimbali zimechukuliwa ikiwemo kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa manispaa hiyo, kuwavua vyeo walimu wakuu 68 wa shule za msingi kwa tuhuma za udanganyifu wa takwimu juu ya elimu bure.

“Licha ya kumuagiza hilo nimemuagiza pia mkurugenzi nafasi hizo 68 za walimu hao wapewe vijana wanaokidhi sifa na wenye uwezo wa kuendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano, tunataka tuwaondoe watumishi wote wenye madaraka ambao bado wanafanya kazi kwa mazoea,” aliongeza.

Aliongeza kuwa, kwa kuwa walimu wa shule za Sekondari, wapo chini ya Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa tayari wamemuandikia katibu huyo barua na kuwaomba awavue vyeo walimu wakuu 22 wa shule za sekondari, waliopeleka takwimu za uongo na kusababisha zaidi ya Sh milioni 70 kwenda kinyume cha matarajio.

Aliongeza kuwa, kila mwalimu mkuu aliyehusika kusababisha ubadhirifu huo wa fedha, atatakiwa kulipa fedha zote kutoka katika mshahara wake.

“Kwanza anashushwa cheo na kuwa mwalimu wa kawaida pili atachukuliwa hatua nyingine kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu lakini tatu atalipa fedha zote zilizopelekwa katika shule yake kinyume na utaratibu kutokana na udanganyifu alioufanya,” alisisitiza Hapi.

Pia Hapi alisema wameshamuandikia barua Mkurugenzi wa Tume ya Utumishi ya Walimu, kuhakikisha hatua nyingine kali za kisheria zinachukuliwa dhidi ya walimu hao.

Wanafunzi hewa

Arusha Mkoani Arusha, walimu wakuu wa shule za msingi 11 na sekondari 12 wamesimamishwa kazi na Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia kwa sababu ya kuongeza idadi ya wanafunzi hewa ili kupata fedha nyingi katika mgawo wa fedha za elimu bure.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mrisho Gambo ameunda timu maalumu kwa ajili ya kuhakiki tena kwa mara ya pili, idadi ya wanafunzi hewa katika shule mbalimbali za serikali walioisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh milioni 26.12.

Kihamia alisema uchunguzi walioufanya awali kupitia waratibu wa elimu, wenyeviti na wajumbe wa Bodi na kamati za shule, wakuu wa shule zote za sekondari, wamebaini kuwa shule 11 za msingi zimeongezewa wanafunzi hewa 907.

Alisema wanafunzi hao hewa wameisababishia serikali hasara ya Sh milioni 23.3 kwa shule za sekondari katika kipindi cha Januari hadi Julai mwaka huu na uchunguzi bado unaendelea ili kubaini shule hizo 11 zilizozidishiwa wanafunzi 907.

“Shule za sekondari idadi imeongezewa jumla ya 942 jambo ambalo halikubaliki hata kidogo na Rais alishasema,” alisema Kihamia na kuzitaja sekondari zilizoongeza idadi ya wanafunzi ni Arusha Day, Baraa, Kaloleni, Kimaseki, Kinana, Morona, Moshono, Naura, Ngarenaro, Oloirieni na Suye.

“Tumegundua wanafunzi hao hewa na hakuna fedha ya serikali itakayoachwa iende kwenye mikono ya watu kiholela holela hapana hivyo nimechukua hatua ya kuwasimamisha kazi na wanahojiwa hao wakuu wa shule pamoja na waratibu wa elimu kata, ikithibitika wamekula hela hizo hatua stahiki zitachukuliwa, kwa nini serikali ikose mapato na hela zipo,” alisema mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake, DC Gambo alisema amepokea taarifa za shule za msingi za serikali 11 zenye wanafunzi ambao hawapo shuleni kulingana na hali halisi ya wanafunzi waliopo darasani na kwamba wanafunzi 907 wanapelekewa fedha wakati hawapo shuleni.

Alitaja shule hizo kuwa ni Azimio, Kimandolu, Magereza, Maweni, Moshono, Naura, Njiro Hill, Olkeryani, Salei, Sokon 1, Terrat na Wema na kwa shule hizo za msingi wameisababishia serikali hasara ya Sh 3,940,008.

Gambo alimwagiza Mkurugenzi wa Jiji kuwachukulia hatua walimu hao, akiwemo Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Hussein Mghewa kujieleza kwa Mkurugenzi amechukua hatua gani kabla ya timu hiyo kuundwa. Pia alisisitiza timu maalumu ya Kamati ya Ulinzi na Usalama, imeundwa ili kubaini wanafunzi wengine hewa.

Imeandikwa na Sophia Mwambe, Dar na Veronica Mheta, Arusha.
Chanzo: Habari Leo

Post a Comment

 
Top