FBI walikabidhi majalada yenye nyaraka hizo juzi na ndani yake kuna barua kadhaa ambazo zinadaiwa kuandikwa na Clinton, akitumia anuani yake binafsi ya baruapepe, wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje.
Wabunge wa Republican waliomba kupatiwa majalada hayo, baada ya FBI kusema kuwa hawana sababu ya kumfungulia mashtaka ya kukiuka itifaki ya mawasiliano, mgombea huyo urais anayewania kumrithi Rais Barack Obama.
Matumizi ya anwani yake binafsi kwa mawasiliano ya kiofisi, yamekuwa silaha kubwa inayotumiwa na wapinzani wake wa kisiasa, wakihoji uwezo wa kuaminika kwa mke huyo wa rais wa zamani, Bill Clinton.
Machi 14, 2012, mjini Washington, Clinton alipata barua pepe kutoka Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ikiwa na kichwa cha habari, siri ikitokea kwa Mnadhimu Mkuu wa Shirika hilo, Dave Petraeus.
Ujumbe huu ni miongoni mwa zaidi ya baruapepe 30,000, pamoja na nyaraka nyingine zilizowekwa hadharani na CIA.
Aidha, ni moja ya maelfu ya ujumbe zilizowekwa alama ya SIRI, ambazo kwa sasa zinafanyiwa uchunguzi, hatua inayoweza kufifisha ndoto za Hillary Clinton za kushinda kinyang’anyiro hicho cha urais.
Barua pepe zilizotoka Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) ni miongoni mwa nyingine 65, zilizowekwa nembo ya siri, ambazo pia hazikuhaririwa kwa umakini. CIA ilisema kuzuiwa kwa baadhi ya barua pepe kulihusiana na sababu za kiusalama wa taifa.
Kuwekwa hadharani kwa barua pepe alizotuma na alizozipokea Clinton kati ya mwaka 2009 na 2013, kulisababisha FBI kuanzisha uchunguzi na kuanza kuwahoji watu wa karibu zaidi na mwanasiasa huyo ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuwa Rais wa Marekani.
Wakati huohuo, wagombea wote wameendelea kuzunguka katika maeneo mbalimbali wakinadi sera zao kabla ya kukutana kwa mara ya kwanza katika mdahalo wa wazi iliopangwa kufanyika mwezi ujao.
Baadhi ya watafiti wanasema kuwa, mdahalo huo ndiyo utakaotoa mwelekeo kwa kweli kuhusu nafasi za wagombea hao.
Post a Comment