0


 Wabunge wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wamelaani mauaji ya mbunge mwenzao kutoka Burundi Bi. Hafsa Mossi yalitokea leo kwa kupigwa risasi katika barabara ya Gihosha, eneo la Nyankoni Jijini Bujumbura.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutokea kwa tukio hilo mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Kikanda na Usuluhishi wa Migogoro kutoka katika Bunge hilo Mhe. Abdallah Mwinyi amesema kuwa, kitendo cha kuuawa kwa mbunge huyo si cha haki hata kidogo kwa kuwa mbunge huyo hakuwahi kujihusisha na migogoro wa aina yoyote katika nchi hiyo.

“Tunalaani kwa nguvu zote mauaji ya mbunge mwezetu kwani ni kitendo cha kinyama na tunatoa wito kwa Waasi kusitisha ghasia na kukaa katika meza ya mazungumzo kutafuta suluhu” Alisema Mhe. Mwinyi.

Kwa upande wake Mhe. Nderakindo Kessy Mbunge wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti Kamati ya Uongozi wa Bunge hilo ameongeza kuwa wamesikitishwa na mauaji hayo ya kikatili aliyofanyiwa Mbunge mwenzao na kuomba haki itendeke na kuwapata wale ambao wamehusika na mauaji hayo na kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Tunasikitika sana na mauaji yalitokea kwa mbunge mwenzetu lakini naahidi kuendeleza yale aliyoyaacha Mhe.Hafsa Kessy hasa katika kupambana katika haki za wanawake na watoto” Alisisitiza Mhe. Nderakindo.

Mhe. Hafsa Mossi aliwahi kuwa Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki katika Serikali ya Rais Pierre Nkurunziza na mtangazaji maarufu wa idhaa ya Kiswahili ya shirika la utangazaji la BBC.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Kikanda na Usuluhishi wa Migogoro, Mhe. Abdallah Mwinyi (kulia) akilaani mauaji ya Mbunge mwenzao Mhe. Hafsa Mosi aliyeuawa na watu wasiojulikana leo 13 Julai, 2016 Mjini Bujumbura. Kushoto ni Mbunge wa Bunge hilo, Mwenyekiti Kamati ya Uongozi, Mhe. Nderakindo Kessy.

Post a Comment

 
Top