Shigela alisema tishio hilo limetokomezwa kwa asilimia zaidi ya 80 ingawa operesheni bado inaendelea katika maeneo mbalimbali, yakiwamo Mapango ya Amboni na misitu inayozunguka Kitongoji cha Mabatini.
Alitoa tamko hilo jana alipokuwa akifungua mkutano wa ushirikiano wa Serikali na asasi za kiraia katika kusimamia utawala bora na maendeleo, ulioandaliwa na mtandao wa Asasi za Kiraia Mkoa wa Tanga (Tasco).
Akisoma hotuba hiyo kwa niaba yake, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa alisema hakuna tena tishio la uhalifu Tanga hivyo, wananchi wafanye shughuli zao kwa amani.
Alisema uhalifu huo ulikuwa njama za kiraia kuvuruga uwekezaji mkubwa uliopo mbioni kufanyika Tanga ukiwamo mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda na kiwanda kikubwa kuliko vyote vya saruji vilivyopo Afrika Mashariki.
Aliziagiza asasi za kiraia kuwajengea wananchi uelewa ili watambue jukumu lao katika kulinda usalama na Tanga iendelee kuwa mahala pazuri kwa kuishi.
Mratibu wa Tasco, David Chanyeghea alisema asasi za kiraia zilisikitishwa na matukio ya kihalifu na kwamba baadhi zilihusika kuwahimiza wananchi kuwafichua wahalifu.
Mbunge wa Mkinga, Danstan Kitandula alisema wakazi wa Tanga wamejengeka katika ustaarabu na ukarimu na kwamba ujio wa miradi hiyo mikubwa utachangia kutoa ajira kwa vijana.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Handeni Vijijini, Ramadhani Diliwa alisema katika kuhakikisha fursa kupitia miradi hiyo inawafikia wananchi, ipo haja kwa kila kiongozi kuwaandaa wananchi.
Post a Comment