Waziri mkuu wa
Israeli Benjamin Netanyahu ametua nchini Uganda katika ziara ya kwanza
kabisa kwa kiongozi wa taifa hilo la kiyahudi kuzuru Afrika tangu mwaka
wa 1987.
Ziara hiyo ya siku 5 imeanzia Uganda, na kisha waziri Netanyahu anatarajiwa kuzuru Kenya, Rwanda na kisha Ethiopia.Ilikuwa kihoja kwa wageni waalikwa kuingia kwenye uwanja huo wa ndege kwani usalama uliimarishwa huku maafisa wa usalama wa Israeli wakishika doria na mbwa na walenga shabaha, mbali na upekuzi wa kawaida wa maafisa wa usalama wa Uganda.
Bw Netanyahu ameandamana na mkewe Sarah na ujumbe wa wafanyibiashara wa sekta mbalimbali za uchumi wa Israeli.
Alipotua katika uwanja huo wa ndege wa Entebbe eneo kulikotokea operesheni ya kipekee miaka 40 iliyopita, ya kuwanusuru mateka wayahudi waliokuwa wametekwa na wanamgambo wa kipalestina, Netanyahu alipata fursa ya kuhudhuria misa ya ukumbusho wa kakake Yoni mmoja wa makomando wa Irsaeli waliokufa katika shambulizi hilo.
Ndege iliyokuwa imewabeba wayahudi hao ilikuwa imetoka Israeli ikielekea Ufaransa.
Kabla ya hapo alikagua gwaride la heshima lililoandamana na makombora 19 kwa heshma yake.
Waziri Netanyahu anasema kuwa ziara hii inalenga kuimarisha uhusiano wa taifa hilo la kiyahudi na mataifa ya Afrika ambayo Israeli inatumai kuwavutia iliwasiwaunge mkono wanaharakati wa Palestina.
Mwenyeji wake rais wa Uganda, Yoweri Museveni, amewakaribisha marais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Paul Kagame wa Rwanda Salva Kiir Mayardit, wa Jamuhuri changa zaidi duniani ya Sudan Kusini Edgar Lungu wa Zambia, rais wa Malawi waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, na waziri wa maswala ya Kigeni wa Tanzania Augustine Mahiga katika kikao cha faragha kinachotarajiwa kujadili maswala ya ugaidi na Usalama wa taifa ambayo Israeli imeahidi kuyasaidia kukabiliana nayo.
Mwandishi wetu aliyeko Kampala anasema kuwa makomando wa Israeli wameshika doria kote mjini Kampala atakozuru Waziri Netanyahu.
Israeli haijakuwa na uhusiano mwema na mataifa ya Afrika ambayo yaliiona kuwa saliti kwa kushirikiana na serikali dhalimu ya Afrika Kusini iliyokuwa ikiwatesa waafrika weusi.
Aidha mataifa ya Afrika yaliunga mkono jitihada za Uhuru wa wapalestina ambao wanakaliwa kimabavu na Isreali na hivyo kutenga taifa hilo la Kiyahudi haswa katika miaka ya 60 na 70 harakati za PLO ziliposhika kasi.
Ziara hii inatarajiwa kupunguza tofauti hizo na kuwapa chambo mataifa ya Afrika iliwalegeze misimamo mikali dhidi ya Israeli.
Post a Comment