Diwani wa viti maalumu shinyanga vijijini Regina Charles akiwa amelazwa kwenye hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga akipatiwa matibabu baada ya kutembezewa kichapo na Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Itubanilo Paulo Msakabili baada ya kutokea ugomvi kwenye kikao cha harusi.
Diwani wa viti maalumu Regina Charels akipatiwa matibabu hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga, ambapo pia alipewa rufaa ya kwenda Bugando jijini Mwanza kupatiwa matibabu zaidi.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Shinyanga vijijini Kiomon Kibamba akimsalimia diwani katika hospitali ya rufaa ya mkoa
*******
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Itubanilo halmashauri ya Shinyanga Paul Msakabili amemshambulia kwa kipigo diwani wa viti maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mengi Charles kata ya Didia wilaya ya Shinyanga na kumjeruhi vibaya na kukimbizwa katika hospitali ya rufaa mkoani Shinyanga.
Tukio hilo lilitokea juzi wakati wakiwa kwenye kikao cha kamati ya maandalizi ya harusi iliyokuwa inafanyika katika kijiji cha Didia wilaya ya Shinyanga baada ya mwalimu huyo kufika kwenye kikao hicho kama mjumbe huku akiwa amelewa na kuanza kufanya vurugu.
Akielezea tukio hilo kwa shida akiwa wodini katika hospitali ya rufaa mkoa wa Shinyanga, diwani huyo alisema wakati wakiwa katika kikao cha harusi ndipo mwalimu Paulo alifika kama mjumbe akiwa amelewa na kuanza kufanya fujo na kelele na kusababisha vurugu.
“Kikao hicho kilikuwa ni cha kamati tendaji ya maandalizi ya harusi na ndipo ilipotolewa hoja na wajumbe kuhusu suala la mapambo na mwalimu Paulo alidai apewe kazi hiyo kwa madai ana mtu wa kufanya kazi hiyo na wajumbe walimtaka amlete huyo mtu ndipo tatizo lilipoanzia”,alieeleza diwani huyo.
Akielezea tukio hilo alisema baada ya kikao hicho cha harusi kuisha ndipo mwalimu huyo alipomfuata na kumkata mtama na kuanza kumshambulia sehemu za kichwani na kumsababishia maumivu makali na kuharibu jicho lake la kushoto.
“Ugomvi uliibuka pale nilipopinga mwalimu huyo kupewa kamati ya mapambo ambapo alidai kunamtu anamfahamu ampe na kumtaka aje na huyo mpambaji iliwajumbe wa kamati tendaji wamuone na kumuhoji pamoja na kufahamu gharama zake lakini Mwalimu huyo alikuja juu na kuanza kunishambulia”,alisema Charles.
Baada ya tukio hilo kutokea diwani huyo alikimbizwa kituo cha polisi Tinde na kupewa fomu namba tatu ya matibabu ya polisi (PF3) kisha kwenda kutibiwa kituo cha afya Tinde ambako alipewa rufaa ya kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga kutokana na kuumizwa vibaya.
Muuguzi wa wodi namba 7 Anjelina Odela alipolazwa diwani huyo alisema alifika akiwa hawezi kuongea huku jicho lake la kushoto likiwa halioni vizuri na magoti yote yamechubuka.
Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali hiyoDkt. Mwita Ngutunya alisema mgonjwa huyo alifikishwa hospitalini hapo akiwa na hali mbaya, ambapo kwa sasa amepatiwa rufaa ya kwenda kupata matibabu hospitali ya Bugando jijini Mwanza baada ya taya yake kuumia.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Graifton Mushi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kuwa mtuhumiwa wanamshikilia na kwamba tukio hilo halihusiani na kazi zao za utendaji ambapo tukio hilo limetokana na kutofautiana wakati wakiwa kwenye kikao cha maandalizi ya harusi.
Post a Comment