0

MKUU mpya wa Wilaya ya Kahama,Fadhili Nkulu,juzi alianza kazi ya wadhifa wake alioteuliwa na Rais John Pombe Magufuli kufanya kazi wilayani Kahama,kwa kuwapiga mkwara wakuu wa Idara katika halmashauri zote tatu kwa kuwazuia kuingia kwenye kikao chake wale ambao walichelewa kufika katika muda uliokuwa umepangwa.
 
Nkulu aliwaita ofisini kwake wakuu wa Idara wote katika halmashauri zote tatu za Mji ,Ushetu na Msalala kwa lengo la kujitambulisha na kufahamiana na walikubaliana kikao hicho kingefanyika saa mbili asubuhi ofisini kwake,lakini kulingana na mazoea yaliyojengeka kwa baadhi ya watumishi baadhi yao walifika zaidi ya saa mbili .
 
Kufuatia hali hiyo Nkulu aliwazuia kuingia kwenye kikao hicho wale waliofika zaidi ya saa mbili na kuwataka wakae nje ya ofisi yake,kwa kuwa makubaliano ya mwaliko huo hayakuwa kufika zaidi ya saa mbili ingawa Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Anderson Msumba alinusulika kwenye mkasi huo,baada ya kufika sekunde chache kabla wakati muafaka wa kikao kuanza.
 
“wewe umefika imezidi sekunde moja baada ya saa mbili wewe ingia wengine watakao kuja kuanzia sasa hawataingia kwenye kikao changu watakaa nje kusubili kutokana na kutotekeleza kufuata ratiba ya vikao “alisema Nkulu ingawa hata baada ya kumaliza kikao chake na wale waliowahi kufika alitoka nje na kuingia kwenye gari na kuendelea na ratiba zake zingine .
 
Hali ya Mkuu huyo wa Wilaya kuwazuia kuingia kwenye kikao chake wakuu wa Idara waliochelewa kufika imepongezwa na umoja wa wazee wa Wilaya ya Kahama,ambapo Katibu wake,Paul Ntelya,alisema kasi hiyo ni nzuri ambayo itawafanya wafanyakazi hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea .
 
Ntelya alimpongeza Mkuu huyo wa wilaya kwa kasi yake hiyo na kumtaka aendelee kuwa mkali kwenye nidhamu ya watumishi wa umma ambao wengi wao wanafika kwenye matukio ya kazi zao kwa muda wanaotaka na si kwa wakati unaotakiwa wengine mpaka hadi ofisini wanafika wanavyotaka.
 
“kwa mfano sisi wazee tulikubaliana kukutana saa nane mchana siku hiyo lakini saa saba na nusu wote tulikuwa tumeshakusanyika iweje wao wakuu wa Idara wakubaliane kukutana saa mbili watu wafike saa tatu mkuu huyo yuko sahihi kabisa kuwazuia kuingia watumishi hao’’alisema Ntelya.
 
Nkulu ameanza kazi kahama katika uteuzi mpya wa wakuu wa wilaya uliofanywa  hivi karibuni na Rais John Pombe Magufuli na kabla ya hapo Mkuu wa Wilaya ya Kahama alikuwa Vita Kawawa aliyeteuliwa mwaka jana wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu na alikuja kushika nafasi ya Benson Mpesya aliyehamishiwa Wilaya ya Songea kabla ya kusitaafu nafasi hiyo mwaka huu .

Post a Comment

 
Top