Mafanikio yoyote katika maisha huwa yanategemea sana nidhamu na tabia
kadhaa ambazo zinaweza kuwa msaada mkubwa kwa muhusika anayehitaji
kuona mafanikio hayo yakitokea katika maisha yake. Mtu yoyote mwenye
kuhitaji mafanikio fulani anahitaji kutengeneza nidhamu pekee
zitakazompa nafasi kubwa ya kufikia mahali husika anapopataka, na hasa
katika ndoto yake. Ni vigumu sana kufanikiwa sawa na wengi wanavyozani
hasa katika maisha yetu, kama hututochukua hatua mbadala na pekee ya
kujenga nidhamu njema zinazoweza kuwa mchango mkubwa katika mafanikio
yetu tunayoyahitaji.
Utakubaliana na mimi ya kuwa; kama unahitaji kufanikiwa katika maisha
na kufikia ndoto yako ni muhimu sana kujenga tabia na nidhamu ya hali
ya juu katika maisha; hasa katika eneo la vitendo na katika kujenga
nidhamu ya kuchukua hatua ndogo kila siku zinazoweza kuwa sababu kubwa
za kukusaidia kufikia ndoto yako uliyonayo. Kumbuka kuwa hakuna
mafanikio yanayoweza kutokea ghafla kwa kulala masikini na kuamka
tajiri, ni lazima uhakikishe unalipa gharama.
Kila mtu unayemwona amefanikiwa katika maisha yake na kuishi katika
kiwango fulani kizuri cha kiuchumi, fedha au kuwa mwenye furaha; hakika
ukifatilia katika maisha ya mtu huyo utakuta ipo gharama aliyoiingia kwa
ajili ya kuhakikisha anailipa na kufikia mahali alipofikia leo hii.
Watu wengi huwa tunapenda sana kufanikiwa ila hatupendi kulipa gharama
za mafanikio tunayoyahitaji; na mojawapo ya gharama zinaweza kuwa ni
kutafuta maarifa na kujifunza zaidi ili kujenga na kuboresha fahamu
zetu, kutokukata tamaa kwa haraka, kukubali kuumia kwa ajili ya kuifikia
na kutimiza ndoto yako.
Katika makala hii ya leo nataka kukusaidia na kukupa ufahamu wa namna
gani ya kujenga hamasa katika maisha yako na kudumu katika hali ya
hamasa hiyo ili kukusaidia kufikia ndoto yako. Huwezi kufikia ndoto yako
kama hutokuwa na sehemu inayokuchochea na kukusukuma katika kufikia
ndoto hiyo. Mojawapo ya siri kubwa niliyojifunza juu ya kufanikisha
jambo lolote lile katika maisha, ni kuhakikisha unalipa kwanza gharama
inayohitajika kulipwa juu ya jambo husika ili uweze kufanikiwa kwa
wakati wake.
Haya ndio mambo 5 unayohitaji kujenga, kuishi na kuyafanya kila siku
ili kuweza kujijengea hamasa na nafasi kubwa zaidi katika kufikia ndoto
yako kwa uharaka.
1: Jenga shauku ya kuifikia ndoto yako.
Kama kweli unahitaji kuwa sehemu ya watu waliofikia katika ndoto zao
na kuwa mashujaa wa kweli wa dunia; tambua hauna budi kuwa na shauku ya
kiwango cha juu cha kufikia ndoto yako uliyonayo. Kumbuka jambo lolote
unalohitaji kufanikiwa katika maisha linahitaji kiwango cha juu sana cha
hamasa kutoka ndani yako ili uweze kulifikia; na kama hautoweka shauku
ya kulifanikisha ni vigumu sana kulifanikisha; hii ni kwa sababu utakuwa
unakosa hamasa ya kutosha ya kukusaidia kukupa mwelekeo wa kule
unapotaka kwenda.
Katika kufanikisha jambo lolote lile likiwemo la ndoto ya maisha
yako, ni muhimu kwanza kujenga tabia ya kuwa na shauku juu ya eneo
husika unalohitaji upate mafanikio hayo. Hakikisha unajenga njaa na kiu
ya kiwango cha juu ya kufanikiwa juu ya ndoto yako. Usikubali kuishi
maisha uliyonayo sasa, usikubali kuwa mtumwa siku zote katikati ya watu
wenye uwezo; amini na wewe una uwezo mkubwa ndani yako; amua kuweka
shauku juu ya ndoto yako, amini utafanikiwa.
2: Jitoe na wekeza zaidi katika kujifunza bila kuchoka.
Angalia ni muda gani unaotumia kila siku katika kujifunza kila siku
mambo mapya ya kukupeleka katika kilele cha mafanikio yako. Mtu mwenye
njaa ya kufanikisha ndoto yake huwa ni mtu anayehakikisha anajifunza
mambo mapya kila siku yanayoweza kuwa msaada mkubwa katika kumpa ujunzi
na uwezo mkubwa na wa kipekee wa kufikia ndoto yake.
Ni vizuri ujenge tabia ya kujisomea vitabu, kusikiliza na kuangalia
mafundisho mazuri ya kukuhamasisha juu ya kufikia ndoto yako. Amua
kuwekeza katika kujifunza kwanza kabla ya kukimbilia kufanya jambo
lolote lile; watu wenye njaa ya kufanikiwa ni watu wenye kujitoa zaidi
katika kujifunza mambo mapya kila siku; ni wasomaji wa viatabu; ni
wasomaji wa makala za kuwahamasisha; ni watu wenye kuhudhuria semina na
warsha mbali mbali za kuwajenga kiakili na kiufahamu ili kufikia ndoto
zao. Fanya hivyo na wewe ili kuweza kukamata nafasi ya juu ya mafanikio
yako na kuweza kufikia ndoto yako uliyonayo.
3: Kuwa mbali na watu wenye kukukatisha tamaa.
Amua kukimbia na kuwa mbali na watu wa namna hii. Kimbia watu wenye
mawazo na mtazamo hasi juu ya ndoto na maono yako mazuri uliyonayo. Wapo
watu wenye tabia ya kukatisha tamaa watu wengine, na ni watu wenye
kukosoa kila kitu kizuri unachoamua kukifanya ilimradi wakuone
hufanikiwi katika maisha yako; na wakati mwingine yawezekana ni watu wa
karibu waliokuzunguka; hakikisha unawakimbia na kukaa mbali nao.
Kuwa karibu na watu wenye tabia na mtazamo hasi juu ya kile
unachotamania kukifanya au kukifikia katika maisha yako, kunaweza kuwa
sababu kubwa ya wewe kutofikia kufanikiwa katika ndoto yako. Watu wa
namna hii wanaweza kukupotezea hamasa na njaa ya kukimbilia katika
kufikia ndoto yako kwa wakati. Amua kuwakimbia na kuwa mbali nao.
4: Usikubali kupoteza muda wako kwenye mambo yasiyo na mchango katika ndoto yako.
Tambua ya kuwa, malengo na mipango mizuri ya kukupa hatua ya kuchukua
kila siku kwa ajili ya kufanikisha ndoto yako ni jambo la muhimu sana,
hasa kwa ajili ya kufanikisha ndoto yako uliyonayo na kukwepa kupoteza
muda kwenye mambo yasiyo ya msingi na faida kwako. Jiwekee malengo
yaliyo wazina yanayofikika (specific and realistic goals)
yatakayokusaidia kufikia ndoto yako pasipo kujichanganya katika kufanya
mambo mengine nje ya kile unachokitaka.
Chagua mambo machache ya kufanya kila siku yatakayokupa hatua na
hamasa kubwa ya kufikia ndoto yako uliyonayo. Usijaribu kufanya kila
kitu katika maisha yako; kufanya kila kitu katika maisha ni kuchagua
kufeli katika kila kitu. Fanya mambo machache kila siku yenye matokeo
makubwa juu ya ndoto yako na ambayo yatakupa hamasa kubwa ya kuendelea
mbele zaidi.
5: Jitie moyo kwa mafanikio madogo unayoyapata na songa mbele.
Kama unahitaji kubaki kwenye hamasa ya kweli ya kukufikisha kwenye
ndoto yako, ni muhimu sana kukubali matokeo madogo unayoyapata kila siku
katika maisha yako. Usikubaliane na udanganyifu wowote wa kimawazo wa
kutokukubaliana na kile kidogo unachokifanikisha; kwa maana katika
kidogo hicho unachopata ni hatua tosha ya kukupa mwelekeo wa kufika
katika mafanikio makubwa zaidi unayoyataka.
Tumia mafanikio madogo unayoyapata kila siku katika malengo yako
uliyojiwekea kama sehemu ya kukupa hamasa na njaa kubwa ya kuendelea
mbele zaidi katika kuifata na kuifanikisha ndoto yako kubwa uliyonayo.
Kumbuka hakuna ndoto isiyowezekana kutimia, ila ni muhimu kujenga
nidhamu mbali mbali zinazoweza kukusaidia kufanikiwa na kufikia ndoto
yako uliyonayo; na nidhamu mojawapo ni kujijengea nidhamu ya
kujihamasisha kila siku ili kufikia ndoto yako nzuri uliyonayo.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.
Post a Comment