0

Mamia ya watu wameandamana jijini
Nairobi, Kenya kupinga mauaji ya kiholela
ambayo yanadaiwa kutekelezwa na
maafisa wa usalama nchini humo.
Maandamano hayo yamefanyika kufuatia
kupatikana kwa miili ya wakili Willie
Kimani, mteja wake Josephat Mwendwa na
dereva wa teksi Joseph Muiruri.
Bw. Kimani na Bw Mwenda walikuwa
wamekodi gari la Bw Muiruri baada ya
kuhudhuria kesi katika mahakama ya
Mavoko 23 Juni, walipotekwa na watu
wanaodaiwa kuwa maafisa wa usalama.
Inadaiwa walizuiliwa kwa muda katika
kituo cha polisi wa utawala cha Syokimau.
Miili yao ilipatikana katika mto wa Ol
Donyo Sabuk, jimbo la Machakos,
mashariki mwa jiji la Nairobi, ikiwa
imefungwa mkono na ikionekana kuwa na
ishara za majeraha.
"Mauaji ya vijana hawa watatu yanafaa
kumtia wasiwasi Rais Kenyatta," amesema
Bw George Kegoro, mkurugenzi mkuu wa
shirika lisilo la kiserikali la Tume ya Haki
za Binadamu Kenya.
"Kiongozi wa nchi ni sharti aunde jopo la
uchunguzi kuhusu kutekwa na kutumiwa
vibayakwa idara za polisi na rasilimali zake
kwa manufaa ya watu binafsi na katika
kutekeleza uhalifu ikiwa ni pamoja na,
katika kisa hiki, mauaji ya kiholela."
Chama cha Wanasheria Kenya
(LSK), kimewashauri wanachama wake
kususia shughuli za mahakama kulalamikia
kuuawa kwa wakili mwenzao, Bw Kimani.
Waandamanaji wameanzia msafara wao
eneo la Freedom Corner, uwanja wa Uhuru
Park na kupitia katikati mwa jiji ambapo
watafika pia makao makuu ya polisi na
makao makuu ya idara ya mahakama.
Baadhi ya mashirika ya kutetea haki za
kibinadamu wanataka Mkuu wa Polisi
Joseph Boinnet na Waziri wa Usalama
Joseph Nkaissery wajiuzulu.
Kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali
linalofuatilia visa vya ukatili wa polisi dhidi
ya raia Kenya la IMLU, mwaka 2015 watu
125 waliuawa kiholela na maafisa wa
polisi.
Kati ya Januari na Aprili mwaka huu, watu
53 tayari wameuawa kwa mujibu wa IMLU.
Maafisa watatu wa polisi waliotuhumiwa
kuhusika katika kutoweka kwa Bw Kimani,
Bw Mwenda na Bw Muiruri wamekuwa
wakizuiliwa na walitarajiwa kufikishwa
kortini leo.

Post a Comment

 
Top