Washtakiwa sita wanaokabiliwa na makosa tofauti yakiwemo ya kubaka, kulawiti na kusambaza picha chafu na za ngono wameendelea kusota rumande kwa kukosa dhamana, baada ya mvutano mkali wa mawakili wa upande wa mashtaka na upande wa washtakiwa kuibuka mahakamani hapo, na hakimu anayesikilisha shauri la dhamana kuahirisha shauri hadi Juni 15 mwaka huu kutoa uamuzi juu ya dhamana.
Miongoni mwa washtakiwa hao, wawili,Iddi Adam Mabena (21) mkazi wa Njombe na Zuberi Thabit (30) mkazi wa Mbarali Mbeya wanaokabiliwa na shtaka la kumbaka na kumlawiti binti mwenye umri wa miaka 21 mkazi wa Wami Dakawa,wilayani Mvomero wanalodaiwa kutenda Aprili 27 mwaka huu majira ya usiku katika nyumba ya kulala wageni ya titii iliyopo wami dakawa wilayani mvomero,shauri lao linalosikilizwa faragha limeahirishwa tena mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya mkoa wa Morogoro Mary Moyo.
Upande wa mashtaka katika shauri hilo linalosikilizwa faragha kwa mujibu wa sheria, umewakilishwa na waendesha mashtaka Gloria Rwakibalila,Edgar Bantulaki,Calistus Kapinga na Mohamed Mkali na limepangwa kufikishwa tena mahakamani hapo Juni 15 mwaka huu kwaajili ya kuanza usikilizwaji wa awali baada ya upelelezi kukamilika.
Uamuzi wa dhamana itolewe ama isitolewe umeshindwa kufikia muafaka baada ya mvutano wa kisheria wa mawakili wa utetezi na wa Jamhuri, katika shtaka la kusambaza picha chafu na za ngono kwa njia ya mtandao kinyume na sheria ya makosa ya mtandao no 14 ya mwaka 2015, linalosikizwa mbele ya hakimu Ivan Msaki,wa Mahakama ya Hakimu mkazi mkoa wa Morogoro,dhidi ya washtakiwa sita,iddi Mabena na Zuberi Thabit,wanaotetewa na wakili Mohamed mkali,na Rajab Salehe,Ramadhani Ally Makunja, Muhsin Ngai na John Peter Thabiti maarufu kama paroko, wakazi wa wami dakawa wilayani Mvomero wanaotetewa na wakili Ignas Punge.
Upande wa mashtaka umeendelea kutetea uamuzi wake wa kuwasilisha kiapo cha kupinga dhamana kwa vile shauri hilo limevuta hisia ya watu, usalama wao utakuwa mashakani wawapo uraiani hasa ikizingatiwa wanadaiwa kudhalilisha utu wa mwanamke na kutoharibu upelelezi kwa vile bado haujakamilika,na kwamba taarifa za kiintelijensia zimebainisha wakiachiwa huru wanaweza wakadhuriwa na jamii.
Hata hivyo upande wa utetezi uliowasilisha hati kupinga kiapo hicho umedai dhamana ni haki ya mshtakiwa,hakuna raia aliyewasilisha kiapo kuhusu hasira kali alizonazo dhidi ya washtakiwa isipokuwa labda ni hisia za mkuu wa upelelezi wa mkoa.
Hakimu Ivan Msaki ameahirisha shauri hilo hadi Juni 15 mwaka huu ambapo uamuzi wa washtakiwa kupewa dhamana au kunyimwa dhamana utajulikana.
Post a Comment