RAIS wa Zanzibar ambaye pia ni Makamu
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Ali Mohamed Shein amewaambia
wafuasi wa CCM kwamba wasihofu, kwani kamwe nchi haiwezi kuondolewa
madarakani kwa kufanya uganga wa kienyeji.
Dk Shein alisema hayo wakati
aliposalimiana na wafuasi wao katika Tawi la Wesha Shengejuu, ambalo
ameahidi kulijenga upya baada ya kuchomwa na watu wanaosadikiwa kuwa
wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF).
Alisema hayo baada ya wafuasi wa CCM,
kudai kwamba viongozi wa CUF wamekuwa wakikesha kucha kutwa wakionekana
kwa waganga wa kienyeji kwa ajili ya kuiroga serikali ing’oke
madarakani.
“Mkipata nafasi waambieni wapinzani
kwamba nchi haiwezi kuondolewa madarakani kwa kufanya uganga wa kienyeji
na kuroga…..,” alisema Dk Shein. Alisema uongozi wa nchi unapatikana
kwa njia ya kushiriki katika uchaguzi unaoitishwa na Tume ya Uchaguzi
kama ndiyo chombo halali kwa mujibu wa Katiba chenye majukumu ya aina
hiyo.
Alisema kwamba CCM kiliamua kuingia
katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa marudio, ulioitishwa na Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutokana na kufutwa kwa uchaguzi wa Oktoba 25.
“Hizo ndiyo njia sahihi ambazo zitamwezesha kiongozi wa nchi kushika
dola baada ya kupata ridhaa kutoka kwa wapiga kura walioshiriki katika
uchaguzi wa marudio,” alisema Dk Shein.
Post a Comment