Maandamano ya kupinga kanuni mpya ya kazi nchini Ufaransa yanazidi kupamba moto huku wafanyakazi kutoka mashirika mbalimbali wakiendeleza migomo.
Marubani wa Shirika la Ndege la Air France wametangaza kufanya mgomo
kati ya tarehe 11-14 Juni kama mojawapo ya hatua za kuunga mkono
maandamano hayo. Mgomo na maandamano hayo yanayoendelea yanatarajiwa
kuathiri watalii na wageni watakaosafiri Ufaransa kwa ajili ya
mashindano ya EURO 2016 yatakayoanza Juni 10 mwaka huu.
Kwa upande mwingine wafanyakazi wa
Shirika la Usafiri wa Reli (SNCF) walioanza mgomo Mei 31 mwaka huu pia
wametangaza kurefusha muda wa mgomo, kufuatia maamuzi hayo ya mashirika
ya usafiri, safari za ndege na treni zinatarajiwa kuathirika kwa kiwango
kikubwa hasa zile zinazoelekea Italia, Uhispania na Ujerumani.
Muungano wa Wafanyakazi wa CGT nchini
humo pia ulitangaza mgomo wa wafanyakazi wa viwanda 19 vya nyuklia na
nishati. Hali hii inatarajiwa kupunguza kiwango cha uzalishaji wa
nishati katika viwanda vya nyuklia nchini Ufaransa.
Kutokana na upungufu huo wa uzalishaji
wa nishati ulioanza jana, viunganishi 125,000 vya umeme vilivyoko
Magharibi mwa nchi vinasemekana kukosa nguvu za umeme. Licha ya hali
hiyo tata kuendelea nchini humo, serikali ya Ufaransa imetangaza mpango
wa kuwasilisha muswada wa kanuni hiyo kwa Baraza la Seneti.
Post a Comment