Madaktari wa
Tanzania katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Moyo ya
Jakaya Kikwete, wakishirikiana na wenzao wa India wamefanikiwa kufanya
upasuaji wa moyo wa aina yake Tanzania.
Upasuaji huo ujulikanao
kama ‘bypass surgery’ ulishirikisha kupandikizwa kwa mishipa ya damu
kutoka sehemu nyingine ya mwili moyoni bila kutumia mashine ya
kusimamisha moyo na mapafu.
Kwa kawaida madaktari wanasema
upasuaji wa moyo hufanyika baada ya moyo na mapafu kusimama, lakini
upasuaji huo ulifanyika wakati moyo na mapafu vikifanya kazi.
Daktari
bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa Bashir Nyangasa ameambia BBC kuwa
upasuaji huo wa kupandikiza mishipa ya damu nje ya mshine ni wa
kihistoria nchini Tanzania.
“Mgonjwa anaweza kutolewa mishipa ya damu kutoka miguuni au mikononi
baada ya kupewa dawa ya usingizi na mishipa hiyo kupandikizwa kwenye
mshipa wa moyo uliokuwa umeziba ili kuruhusu mzunguko wa damu wa moyo
kama kawaida bila kutumia mashine,” amesema.
Upasuaji huo wa moyo
kwa njia ya kupandikiza umefanyika kwa watu wawili, ambao umeonesha
mafanikio makubwa kwa kuwa hali zao zinaendelea vizuri .
Dkt
Nyangasa amesema kwa sasa hakuna haja ya Watanzania wenye matatizo ya
moyo kwenda nje ya nchi kwa kuwa wao kama wataalam wameweza kufanya
upasuaji huo.
Anasema madaktari sasa wanaweza kuhudumia wagonjwa wengi zaidi wenye
uhitaji na kupunguza gharama kwa serikali ya kusafirisha wagonjwa wa
moyo nje ya nchi.
Mwandishi wa BBC aliyepo Dar es Salaam Esther
Namuhisa anasema wengi wa wagonjwa wamekuwa wakisafiri hadi India ambapo
wengi hukumbana na changamoto nyingi kupata huduma hiyo kifedha na hata
kwenye upande wa lugha.
Post a Comment