0

KILIMO CHA UYOGA 
Uyoga ni chakula kizuri sana na chenye virutubisho vingi vinavyohiajika katika mwili wa mwanadamu, Wataalumu wengi wa afya na tiba wanautumia katika kutibu magonjwa mbalimbali kwa mwanadamu, Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa uyoga unavitmini za kutosha pamoja na protini.

 Miaka ya karibuni, utaalamu wa kuotesha uyoga umeanza hapa Tanzania baada ya watu kutilia maanani lishe bora ya protini na manufaa mengine ya zao hilo.

Kwa kuwa uyoga upo wa aina mbalimbali, usitawishaji wake hutofautiana katika mahitaji yake, ikiwa ni pamoja na hali ya hewa, malighafi za kuoteshea, urahisi wa teknologia ya kuotesha katika mazingira ya Tanzania na soko lake kwa wananchi na katika hotel mbalimbali.

Hata hivyo ni wananchi wachache tu wanaojua jinsi ya kuulima inavyopaswa na pia ni wachache wanaoweza kutofatifa aina mbalimbali za uyoga na upi unafaa kuliwa na upi haufai kwa kuliwa.

Anaanza kuueleza kuwa ,  kwa Tanzania aina zinazofaa ni zile ambazo hustawi vizuri, kwenye maeneo ya joto la wastani wa nyuzi joto 20C hadi 33C. Aina hizi za uyoga pia uhitaji hali ya unyevu hewani (moisture) wa kiasi cha asilimia 75%. Kwa mfano uyoga aina ya mamama.                          

Ujenzi wa banda uyoga

UOTESHAJI WA UYOGA
 Ikiwa unahitahitaji kuanza kuotesha uyoga, inabidi kwanza uwe na chumba chenye paa ambalo litazuia jua, mvua, na vumbi.

Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa uyoga. Mkulima wa kawaida anaweza kutumia kasha kama sehemu ya giza,

Mara Nyingi mbegu za uyoga huzalishwa kwenye maabara zenye vifaa vinavyowezesha kuotesha mbegu hizo bila kuchafuliwa au kuchanganyika na vimelea kama bakteria, ukungu au jamii nyingine za uyoga ambazo haziliwi,

Tanzania hivi sasa maabara hizo zipo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo(SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kituo cha utafiti wa kilimo-Uyole na taasisi ya utafiti wa kilimo cha bustani- Tengeru (HORTI –Tengeru, Arusha),

 HATUA MUHIMU ZA KUZINGATIA WAKATI WA KUOTESHA UYOGA 
Baada ya kupata mbegu ni kama ifuatavyo:
• Kusanya masalia ya mazao kama vile mabua, majani ya mpunga, ngano, pumba za mpunga au mahindi, masalia ya miwa baada ya kukamua nk. Vitu hivi hutumika kama mali ghafi kwa kuoteshea uyoga.
 • Mabua, majani ya mpunga au migomba yakatwe kwa urefu usiozidi sm 6, au urefu wa vidole kwa kutumia panga au kisu.
• Loweka mali ghafi kwenye maji ya kawaida kwa muda wa siku nzima (masaa 24).
• Kisha yachemshe kwa muda wa saa mbili ili kuua vijidudu pamoja na vimelea vilivyomo.
• Ipua na umwage maji yote halafu tandaza kwenye kichanja kisafi ili yapoe bila kuchafuliwa na vumbi au vijidudu.
• Kisha jaza mali ghafi hii katika mifuko ya nailoni tayari kwa kupanda mbegu.

NAMNA YA KUPANDA 
Kuna aina mbili za upandaji

AINA YA KWANZA 
Chukua mfuko wa nailoni wenye upana wa cm 40 - 45 na kimo cm 75.
Weka tabaka la mali ghafi ya kuoteshea yenye kina cha sm 10 katika mfuko halafu tawanya mbegu ya uyoga juu yake.

Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya vioteshea na kuweka mbegu juu yake. Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifike ujazo wa robo tatu ya mfuko.                            
AINA YA PILI 
Changanya malighafi ya kuoteshea (baadaya kuchemshwa na kupoa) na mbegu ya uyoga katika uwiano wa 1: 25 (mbegu : malighafi ya kuoteshea) kwa uyoga aina ya mamama (Pleurotus spp.)Kisha mchanganyiko huo ujazwe katika mifuko ya nailoni mifuko hii iwe na ukubwa wa cm 20 kwa cm 40 ambamo unaweza kujaza kilo 1 – 1.5 ya malighafi ya kuoteshea.

Funga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye  kipenyo cha cm 1 kwa kila umbali wa cm 6 hadi 10 kwa kila mfuko.

Matundu yawe mengi ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko. Kumbuka uyoga ni kiumbe hai hivyo unahitaji kupumua kama inavyoonekana kwenye picha hapo chini.

MATUNZO YAKE 
Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa kawaida waweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza.

 Acha mifuko humo kwa muda wa siku 14 - 21 bila kufunua ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri.

Utando wa uyoga ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya kuoteshea, hamishia kwenye chumba chenye mwanga na hewa ya kutosha kisicho pigwa na jua. Katika chumba chenye mwanga, mifuko inaweza kuwekwa kwenye, meza, chanja la waya au miti.

Mifuko inaweza pia kuning’inizwa kwenye kamba toka kwenye boriti za paa la chumba hicho. Unatakiwa kudumisha hali ya unyevu kwenye chumba hicho cha mwanga kwa kumwaga maji sakafuni.

Ukiona vipando vinakauka unaweza kunyunyizia maji yaliyochemshwa na kupoa juu ya mifuko mara tatu au zaidi kwa siku.

Tumia bomba la mkononi lenye ukubwa wa lita moja kunyunyizia maji. Tafadhali: usizidishe maji kwani maji yakiwa mengi sana yaweza kuozesha uyoga uliyoanza kuota. Aina nyingi za uyoga huanza kutoa vichwa (pini) siku 2 - 3 baada ya kuwekwa kwenye mwanga.

JINSI YA KUVUNA UYOGA 
Uyoga huwa tayari kuchumwa siku tatu baada ya vichwa /pini kuonekana. Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga kisha zungusha hadi uyoga ung’oke.

Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwani kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea. Mkulima anatakiwa ajue soko la uyoga kabla ya kuvuna ili kuepuka gharama za kuhifadhi. Kwani uyoga ukishavunwa unatakiwa uliwe kabla haujaharibika.

UHIFADHI WA UYOGA
 i) Unaweza ukauweka uyoga kwenye mifuko ya karatasi na kuhifadhi kwenye jokofu.
ii) Unaweza ukauanika juani hadi ukauke na kuweka kwenye mifuko ya nailoni liyofungwa vizuri ili isipitishe hewa na unyevu.

SOKO LA UYOGA 
i) Watu wengi hupenda uyoga mbichi uliotoka shambani wakati huo huo kama kitoweo, kwa kutumia kama nyama, samaki, au kama kiungo.
ii) Unaweza kuuza uyoga mbichi kwa bei ya shilingi 3000/= hadi 5000/= kwa kilo kwa uyoga aina ya mamama. Pia unaweza kuuza nje ya nchi ikiwa uyoga wako ni kiasi kikubwa na uko katika viwango vinavyo kubalika kimataifa.

MAMBO YA KUZINGATIA
 • Uzalishaji wa uyoga huzingatia sana hali ya hewa na vifaa ulivyonavyo, hivyo basi, kabla hujachagua aina ya uyoga unaotaka kupanda pata ushauri kwa wataalamu walio karibu nawe.
 • Ukishanunua mbegu, kama hupandi kwa muda huo, hakikisha umehifadhi mbegu hiyo kwenye jokofu. Kama huna jokofu la kuhifadhia, nunua mbegu baada ya kuandaa kila kitu. Hata hivyo, uotaji wa mbegu huwa mzuri kama zitakaa nje ya jokofu kwa siku mbili.
• Mbegu za uyoga huwekwa ndani ya chupa yenye ujazo wa mililita 300, waweza kutumia chupa moja katika kupanda kwenye kilo 15 ya mali ghafi ya kuoteshea. Hakikisha unamaliza mbegu yote iliyo ndani ya chupa kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.
• Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu ambayo siyo nyeupe ni dalili za maambukizo ya vimelea vingine na hivyo haifai kwa kupanda.
• Hakikisha chumba cha kupandia ni kisafi na hakipati vumbi toka nje ili kuzuia maambukizo ya magonjwa ya uyoga.
• Usimwagilie uyoga maji yasiyochemshwa kwani maji hayo mara nyingi si salama. Yaweza kusababisha vimelea vingine kuota, kwani uyoga ni dhaifu kuhimili ushindani wa vimelea.
• Pia waweza kusababisha magonjwa ya uyoga ambayo kutibu kwake kunahitaji kutumia dawa za viwandani ambazo ni sumu na hivyo kusababisha madhara kwa mlaji. Unaweza kupata faida nyingi kutokana na uzalishaji wa uyoga,

FAIDA ZA UYOGA:
- Lishe kama protini inayolingana na ile ipatikanayo kwenye maziwa, samaki na kunde.
 Pia utapata vitamini B, C, na D, na madini ya joto, phosphoras, chuma na potashi.
• Uyoga husadikika kutibu maradhi kama kifua kikuu, kisukari, moyo, shinikizo la damu na figo.
• Masalia ya mazao hutumika katika kuzalishia uyoga, na baada ya kilimo cha uyoga yanaweza kutumika kama mbolea asili kwa kilimo cha bustani. Masalia ya kilimo cha uyoga pia hutumika kama chakula cha mifugo kama ng’ombe.
• Kilimo hiki huhitaji eneo dogo sana la ardhi na kiasi kidogo cha maji, hivyo hupunguza tatizo la ukosefu wa ardhi na ugomvi katika jamii ambao unatokana na tatizo hilo.
•  Mama W. Marwa alimalizia kwa kusema kuwa, Kilimo hiki ni njia nyepesi ya kutoa ajira kwa familia kutokana na gharama ndogo, teknolojia rahisi inayotumika na pato lake ni kubwa, hivyo kupunguza utegemezi kwa familia na umaskin pia hasa kwa atayetilia maanani na mkazo katika kulima uyoga.

Post a Comment

 
Top