Watanzania wengi hawana ndoto ya kwenda kufanya kazi ughaibuni,
kuepukana na umaskini. Lakini mwandishi Anaclet Rwegayura anahoji, iwapo
uchumi wa taifa hilo unaweza kufikia tabaka la kati.
Mafundi na wote wafanyao kazi za sulubu katika nchi hii wanaendelea na
shughuli zao za kawaida bila hata chembe ya tamaa kwamba siku moja
wangehesabiwa miongoni mwa matajiri au wafanyabiashara wakubwa. Lengo
lao ni kuweka maisha yao katika usawa na ulimwengu.
Sehemu ndogo ya watu inayopata fursa ya ajira, aghalabu katika maeneo ya
mijini, hutaka wawe na kipato cha hakika. Kwa desturi, wakazi wa
vijijini walifaidika kwa njia mbalimbali kwa kuwa na jamaa zao
waliobahatika kupata ajira mijini. Ulikuwa mfumo mzuri wa maisha wenye
wafanyakazi wakaao mijini wakifadhili ustawi wa familia za vijijini na
maendeleo ya vijijii vyao.
Hivi karibuni, hata hivyo, hali hiyo imekuwa shaghalabaghala. Mahusiano
ya kiuchumi yaliyokuwepo kwa muda mrefu kati ya familia za vijijini na
wafanyakazi waishio mijini imebadilika ghafla kila upande ukijizatiti
peke yake ili uendelee kuishi.
Jamii za vijijini zimeathirika sana kutokana na kupungua kwa mazao
yauzwayo nchi za nje kama vile kahawa, chai, pamba, korosho, nyama na
mengine mengi kutokana na, baadhi ya sababu, kushindwa kwao kukidhi
matakwa ya ushindani wa masoko ya kimataifa.
Mazao mengi bado hayajafikia viwango vilivyowekwa, ikiwa pamoja na vya
kulinda afya za walaji, usafi na usalama ili viweze kupata hati za
kuruhusiwa viingizwe, kwa mfano, katika soko la Ulaya.
Kiwango kidogo cha mapato ya mazao yauzwayo nje ya nchi, hasa kutokana
na sekta ya kilimo, yanamaanisha uwezo mdogo wa serikali na hata sekta
binafsi kuboresha mishahara ya wafanyakazi. Hali hii itakuwa ngumu zaidi
kutokana na urahisi wa watafuta ajira kuhama katika nchi sita wanachama
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika ujumbe unaotangazwa kila siku na vituo vya televisheni, Rais John
Pombe Magufuli anawahimiza Watanzania wawe na tabia ya kulipa kodi
katika shughuli zote za biashara na mapato.
Akihutubia kwa mara ya kwanza mkutano wa hadhara wa Siku ya Wafanyakazi
Duniani mwaka huu, Rais Magufuli alitamka: “Nchi yetu haitaweza kufikia
uchumi wa kati unaoendeshwa kwa viwanda kama tutaendelea kulea uvivu,
uzembe, ubadhirifu, rushwa, ukwepaji kodi, kutotimiza wajibu wetu na
wafanyakazi hewa.“
Maovu yote haya, kama hayakuachwa, yatamaliza uchumi na kupeleka nchi
katika hali ya kugutusha. Hakuna mtu atakuwa na fursa ya kuwa na kipato
kizuri na endelevu. Wafanyakazi wengi hawatakuwa na muda wa mapumziko,
kutunza maisha ya familia zao na hata michezo ambayo husaidia kutunza
afya zao kimwili, kimawazo na kisaikolojia.
Katika baadhi ya nchi ambazo, kwa bahati mbaya, zimekuwa na uongozi
usiofaa, vizazi vimesambaratika kutokana na uchumi duni. Je, ni
Watanzania wangapi wanatambua hilo?
Hotuba ya rais ilimfanya kila mfanyakazi afumbe na kufumbua jicho baada
ya kuwapunguzia asilimia 2 katika kodi inayokatwa katika mishahara yao
kuanzia Mei 2016.
Lakini agizo hilo la rais halikufunga mjadala katika asasi mbalimbali
juu ya kiwango gani cha mshahara kinastahili kwa maisha ya mfanyakazi
katika mazingira yanayobadilika ya uchumi wa dunia ambapo umaskini
unaendelea kuwa adui asiyekamatika kwa Watanzania.
Wakati huu, nchi inakabiliwa na udhaifu na vikwazo vingi ambavyo vinatishia ukuaji wa uchumi.
Mbali ya kupambana na ufisadi, uboreshaji wa kuonesha matokeo ya kazi za
serikali na kuhimiza utawala wa sheria, miongioni mwa mambo mengine,
hapana budi vyama vya wafanyakazi vishirikishwe kikamilifu pamoja na
waajiri na bodi za mazao kutathmini tofauti za mishahara na kuwezesha
wazalishaji na wafanyakazi wawe na tija ya juu kabisa.DW
Post a Comment