0

ALIZETI ni zao mojawapo kati ya mazao muhimu yanayotoa mbegu za mafuta. Hutoa mafuta kati ya asilimia 40 – 45 na mashudu yake ni chakula cha mifugo.

Alizeti huvumilia ukame na hulimwa kwa ajili ya biashara na matumizi ya nyumbani. Wakulima huvuna kiasi kidogo kati ya gunia tatu hadi tano kwa hekta. Hapa nchini alizeti inastawi maeneo mengi hususani maeneo yote yanakostawi mahindi. Baadhi ya mikoa inakostawi sana alizeti ni pamoja na Singida, Sumbawanga, Mbeya, Iringa, Ruvuma, Mtwara, Tanga na Dodoma.

Zao hilo hushambuliwa na magonjwa ya majani, mizizi na masuke ambayo husababisha upungufu wa mavuno. Mtafiti Mkuu na Mtaalamu wa magonjwa ya virusi vya mmea kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo Mikocheni, Dk Joseph Ndunguru anasema Tanzania ni nchi mojawapo ambayo inazalisha alizeti na mabaki yake hulisha mifugo.

Ndunguru anasema zao hilo lililetwa nchini na wakoloni, likaonekana linaweza kupandwa maeneo mengi nchini. Anasema alizeti inalimwa na wakulima wadogo wadogo ambapa asilimia 50 za zao hilo hulimwa mkoani Dodoma. Anasema mahitaji ya mafuta ya kula ni tani 219000 kwa mwaka pia inaweza kuwa zaidi ya hapo.

“Mahitaji ya alizeti yanaongezeka kila mwaka. Mazao ya mafuta nchini karanga hutoa asilimia 40, alizeti asilimia 36, ufuta asilimia 15, pamba asilimia 8 na michikichi asilimia moja,” anasema Ndunguru. Kwa mujibu wa Ndunguru, wastani wa uzalishaji wake upo kati ya tani 75,000 mpaka tani 100,000, ambapo mwaka 2001 mpaka 2005 ulikuwa hivyo.

Anasema mwaka 2006 uzalishaji ulikuwa tani laki 3.5. ongezeko hilo limetokana na ubora wa mbegu ukitokana na ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya kimataifa na asasi zisizokuwa za serikali, pamoja na kuwepo kwa sheria ya mbegu ya mwaka 2003 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2007. Mtafiti huyo anasema kuna ugonjwa wa majani wa alizeti ambao unasababishwa na virusi, unaitwa batobato ambao unaleta upotevu wa hadi asilimia 58-87.

Anasema ugonjwa huo unaenezwa na wadudu mbalimbali wa aina mbili, hujulikana kama vidukari na inzi weupe. Dalili za ugonjwa huo: Mimea iliyoathiriwa hudumaa, majani hupoteza rangi ya kijani kibichi na kuwa njano hasa kwenye mishipa ya majani. Vile vile majani yanapungua ukubwa wake na hujikunja mithili ya batobato.

Pia sehemu ya juu ya mmea ulioathirika huwa na mlundikano wa maji. Anaeleza njia za kudhibiti ni kuzalisha mbegu zenye ukinzani, kuondoa magugu shambani ambayo yanaweza kuhifadhi wadudu wanaoeneza huo ugonjwa. Anaeleza kuwa ugonjwa huo upo katika nchi mbalimbali, hapa nchini upo katika wilaya ya Karatu.

Ndunguru anasema kazi ya utafiti inaendelea kwenye maabara ya utafiti Mikocheni ili kubaini aina ya virusi hivyo. “Utafiti umeanza mwezi huu, mwishoni mwa mwaka utakuwa umekamilika,” anasema mtafiti huyo. Anasema njia wanayotumia kudhibiti ugonjwa huo ni kuwaelimisha wakulima na maofisa ugani juu ya ugonjwa huo ili usiendelee kusambaa.

Pia anasema utafiti utakaofanywa utabaini aina ya virusi, kuainisha maeneo ambayo ugonjwa umeenea hapa nchini. “Ili kufanikisha hilo tunahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, halmashauri, asasi zisizo za serikali na wizara ya kilimo,” anasema Ndunguru. Anaeleza faida za alizeti ni kutengeneza mafuta na mashudu kwa ajili ya malisho ya mifugo.

Haya ni mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa uzalishaji wa alizeti. Anasema kwanza mkulima anapaswa achague aina bora ya mbegu inayovumilia magonjwa, wadudu, inayotoa mazao mengi na kiwango kikubwa cha mafuta. Pia mbegu inayokomaa kwa wakati mmoja ili kurahisisha uvunaji.

Ili kupata mazao mengi na bora inapaswa mkulima arutubishe udongo kwa kutumia mbolea za mboji na samadi. Maandalizi yake wakati wa kuvuna: Ni vyema kukagua shamba kuona kama alizeti imekomaa. Alizeti hukomaa kati ya miezi minne hadi sita tangu kupanda. Wakati huo punje huwa na unyevu wa asilimia 25.

Ni muhimu kuvuna alizeti mapema ili kuepuka mashambulizi ya panya, mchwa na ndege waharibifu. Dalili za alizeti kukomaa: Suke hubadilika rangi kutoka manjano na kuelekea kuwa nyeusi, pia viua vya pembeni mwa suke hunyauka na hubadilika kutoka rangi ya manjano na kuwa ya kahawia. Uvunaji, ukaushaji na ubebaji wake: Vifaa vya kuvunia na kubebea kutoka shambani ni visu, vikapu, magunia, matenga vifaa vya kukaushia, maturubai, mikeka, vyombo vya usafiri kutoka mashambani, matoroli, matela ya matrekta na mikokoteni ya kukokotwa na wanyama.

Alizeti huvunwa kwa kutumia kisu, nchi zilizoendelea hutumia mashine za kuvunia zao hilo. Kukausha: Kuna hatua mbili za kukausha alizeti; kukausha masuke na kukausha mbegu za alizeti. Kukausha masuke Masuke hutandazwa kwenye kichanja bora katika kina kisichozidi sentimita 30 ili yaweze kukauka vizuri.

Vilevile huweza kutandazwa kwenye maturubai, mikeka au sakafu safi. Lengo la hatua hii ni kukausha masuke ya alizeti ili kurahisisha upuraji. Upuraji hufanyika baada ya kuhakikisha kuwa masuke ya alizeti yamekauka vizuri. Masuke ya alizeti hupurwa kwa kutumia mikono ambapo mbegu hutenganishwa kwa kupiga masuke taratibu kutumia mti.

Ni muhimu kupiga masuke taratibu ili kuepuka kupasua mbegu Mbegu zilizokauka vizuri Kufikicha mbegu maganda yake hutoka kwa urahisi zinapofikichwa. Kumimina kwenye chombo kama . Pia hutoa mlio mkali zinapomiminwa kwenye vyombo hivyo, Mbegu zilizokauka hung’ara.

Kutumia kipima unyevu Alizeti iliyopurwa huhifadhiwa katika hali ya kichele kwenye maghala bora, yaani vihenge, sailo au bini. Alizeti ya kuhifadhi kwenye maghala ya nyumba ifungashwe kwenye magunia na ipangwe kwenye chaga kwa kupishanisha. Ili kurahisisha kazi ya kukagua ghala, acha nafasi ya mita moja kutoka kwenye ukuta.

Ziba sehemu zote za ghala ili kuzuia panya kuingia. Panya hupenda sana kula punje za alizeti, na husababisha upungufu mkubwa wa punje ambao husababisha upotevu wa asilimia 30 kwa kipindi cha miezi mitatu ya hifadhi.

Asilimia ya upotevu inaweza kuwa kubwa zaidi kutegemea idadi ya panya na upatikanaji wa vyakula vingine kwa wakati huo. Matumizi ya mbegu za alizeti Mbegu za alizeti hasa zenye mistari zinaweza kuliwa baada ya kukaangwa au kukaushwa.

Post a Comment

 
Top