Simba aliyetoka katika mbuga ya taifa ya wanyama ya Nairobi amemshambulia mzee mmoja jijini humo mapema asubuhi.
Simba huyo alitoka mbugani na kuonekana karibu na eneo la City Cabanas, katika ya Mombasa Road.Afisa wa mawasiliano wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) Bw Paul Udoto ameambia BBC kwamba mzee aliyejeruhiwa ni wa umri wa miaka 63 na amepewa matibabu ya dharura katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta kisha akakimbizwa hospitalini kwa matibabu kamili.
Hata hivyo, Bw Udoto amesema mzee huyo hayuko hatarini.
Kwa mujibu wa afisa huyo, simba huyo huenda alikerwa na kelele za magari yaliyokuwa yakipita.
Vikosi vitatu vya maafisa wa KWS vilitumwa kumdhibiti na kwa mujibu wa Bw Udoto, simba huyo anaelekezwa ndani kwenye mbuga.
Maafisa wanaendelea kushika doria kubaini iwapo kuna simba wengine walitoka mbugani.
Visa vya simba kutoka mbugani vimekuwa vikiripotiwa siku za karibuni. Mwezi mmoja uliopita, simba wanne waliingia maeneo ya makazi eneo la Langata.
Wiki mbili zilizopita, simba wawili walidaiwa kuonekana karibu na barabara ya Ngong.
Post a Comment