Wanajeshi wawili wa
Marekani na afisa mmoja wa Afrika Kusini wameuawa kwa kupigwa risasi
katika kituo cha kutoa mafunzo kwa maafisa wa polisi nje ya mji mkuu wa
Jordan, Amman, maafisa wa usalama wamesema.
Kituo hicho
kinachofadhiliwa na Marekani katika mtaa wa Muwaqqar, viungani mwa mji
wa Amman, hutumiwa kutoa mafunzo kwa maafisa wa polisi wa Iraq na
Palestina.Msemaji wa serikali ya Jordan Mohammad Momani amesema mshambuliaji huyo aliwajeruhi Wamarekani wengine wanne na Wajordan wanne kabla ya kuuawa na maafisa wa polisi wenzake.
Bw Momani ameambia shirika la habari la Petra kwamba kisa hicho kinachukuliwa uhalifu na kwamba uchunguzi umeanzishwa.
Afisa wa polisi aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa mkufunzi wa ngazi ya juu wa cheo cha kapteni, afisa mmoja wa Jordan alinukuliwa na shirika la habari la Reuters.
Haijabainika ni nini kilichochochea shambulio hilo.
Ubalozi wa Marekani katika mji wa Amman uliandika kwenye Twitter kwamba umepokea habari kuhusu kicha hicho.
"Tunawasiliana na maafisa husika wa serikali ya Jordan, ambao wameahidi kusaidiana nasi kikamilifu."
Kisa hicho kimetokea wakati wa makumbusho ya miaka 10 tangu kutekelezwa kwa mashambulio ya mabomu na kundi la al-Qaeda katika hoteli tatu mjini Amman, shambulio lililoua watu 50.BBC
Post a Comment