0
 
Diack anachunguzwa kwa tuhuma za ulaji rushwa
Shirikisho la riadha duniani IAAF leo litapokea matokeo ya uchunguzi huru kuhusu madai ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli miongoni na ufisadi mwa wanariadha Urusi.
Tume huru, iliyoundwa na shirika la kukabiliana na matumizi ya dawa zilizoharamishwa (Wada), itachapisha matokeo hayo saa 14:00 GMT.
Ripoti hiyo itaonyesha "ngazi tofauti ya ufisadi", na hata kulinganishwa na Fifa, mmoja wa waliochangia kuandika ripoti hiyo, Bw Richard McLaren amesema.
Lord Coe, rais wa IAAF amekiri kwamba hizi ni “siku za giza kwa mchezo huo”.
Kwenye mahojiano na BBC Radio 5 Coe ameongeza: "Siku moja baada yangu kuchaguliwa, nilianzisha utathmini mkubwa. Kutokana na madai ambayo yametolewa, utathmini huu umeharakishwa.
“Nimejitolea sana kurejesha Imani katika mchezo huu. Hata hivyo, hii ni safari ndefu.”
McLaren, ambaye ni mwanasheria, ameambia BBC World Service kwamba tume hiyo huru ilikuwa na jukumu la kubaini ukweli kuhusu madai yaliyotolewa kwenye makala moja ya televisheni ya Ujerumani kuhusu wanariadha wa Urusi mwezi Desemba.
Makala hiyo ilidai maafisa wa Urusi walipokea pesa kutoka kwa wanariadha ili kuwapa dawa zilizoharamishwa na kuficha ukweli wakati wa kupimwa kwao. Maafisa wa IAAF walihusika katika kuficha ukweli.
  Coe
Coe amekiri hizi ni siku za giza kwa mchezo wa riadha
Rais wa Wada Sir Craig Reedie, pia aliambia BBC Radio 5 kwamba ripoti hiyo itakayotolewa Jumatatu: “Nafikiri itakuwa thabiti kuhusu yale tume hiyo iliundwa kukamilisha, ambayo ni kuchunguza madai ya ukiukwaji wa sheria za kuzuia matumizi ya dawa zilizoharamishwa Urusi, na jamii ya kukabiliana na dawa hizi pamoja na wadau katika mchezo huu kwa jumla wanafaa kuwa tayari kwa hili.”
Lamine Diack, 82, rais wa zamani wa IAAF, tayari anachunguzwa kwa tuhuma za ufisadi na ulanguzi wa pesa.
Coe, anayetoka Uingereza, alikuwa makamu wa rais wa shirikisho hilo kwa miaka minane kati ya 16 ambayo Diack alikuwa kwenye usukani.
Hata hivyo amesema hakufahamu lolote kuhusu tuhuma zilizowasilishwa dhidi ya raia huyo wa Senegal, aling’atuka Agosti, hadi zilipotangazwa hadharani mwanzoni mwa wiki iliyopita.
“Hiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kuyasikia madai hayo na nina uhakika hata kwa watu wengi katika mchezo huu ni vivyohivyo.”
Wakati wa kuchaguliwa kwake, Coe aliyeshinda Olimpiki mbio za 1500m mara mbili alimtaja Diack kama “kiongozi wa kidini wa IAAF lakini alikiri Jumapili kwamba huenda akashutumiwa kwa madai hayo.
Hata hivyo alisema: “Lakini huko ni kudhani kwamba nilifahamu tuhuma hizi zozote nikisema hayo, jambo ambalo si kweli.

Post a Comment

 
Top