RAIS John
Magufuli ambaye tangu Novemba 17, mwaka huu alikuwa katika Ikulu ya
Chamwino mkoani Dodoma kwa majukumu mbalimbali, amerejea Dar es Salaam
jana na wakati wowote inaelezwa kwamba anaweza kutangaza Baraza la
Mawaziri linalosubiriwa kwa hamu na Watanzania.
Dk
Magufuli alitua Ikulu ya Chamwino, Novemba 17 kwa kutumia usafiri wa
barabara akisafiri kwa zaidi ya kilometa 300 kwenda katika Makao Makuu
ya Serikali ambako kwanza alikuwa na majukumu mawili makubwa.
Novemba
19, mwaka huu, alimteua Mbunge wa Ruangwa mkoani Lindi, Majaliwa Kassim
Majaliwa kuwa Waziri Mkuu na siku iliyofuata alimwapisha katika Ikulu
hiyo iliyoko takribani kilometa 40 kutoka Dodoma Mjini.
Aidha, baada ya kumwapisha Majaliwa asubuhi, jioni hiyo ya Novemba 20,
Dk Magufuli aliyeingia madarakani Novemba 5, mwaka huu, alilihutubia na
kulizindua Bunge la 11 mjini Dodoma katika hotuba iliyosisimua wabunge
na Watanzania kwa ujumla kwa kugusa kero na mipango mbalimbali
anayokusudia kuifanya.
Dk
Magufuli alirejea Dar es Salaam huku tetesi zikiimarika kwamba
atatangaza baraza lake la mawaziri siku yoyote kuanzia jana, na
aliondoka Dodoma kwa ndege majira ya saa mbili asubuhi.
Kuwapo
kwake kwa siku nyingi katika kijiji cha Chamwino akifanya kazi,
kulipongezwa na wanakijiji hao. Aidha, wanazuoni na wanasiasa
walitafsiri uwapo wake kijijini hapo kuwa ni kujichimbia asibughudhiwe
wakati akipanga baraza lake la mawaziri na mfumo wa uendeshaji mpya wa
baraza hilo.
Na ishara
au dalili kwamba Baraza la Mawaziri limeiva au litatangazwa wakati
wowote ni hatua ya Dk Magufuli kutua Dar es Salaam na baadaye mchana
kwenda ofisini kwa Majaliwa ambako ni jirani na Ikulu ya Magogoni.
Kwa
mujibu wa Katiba ya Tanzania, Rais atateua Baraza la Mawaziri kwa
kushauriana na Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, hivyo kuna kila dalili
wawili hao kama sio wote watatu, wameshafanya kazi hiyo. Ofisi ya Waziri
Mkuu ilithibitisha Dk Magufuli kutinga ofisini kwa Waziri Mkuu,
Majaliwa na kufanya mazungumzo ya takribani saa moja.
“Rais
aliingia ofisini kwa Waziri Mkuu Majaliwa majira ya saa tisa na kulakiwa
na mwenyeji wake na baadaye walikaa kwa mazungumzo yao wawili tu.
“Baada ya mazungumzo hayo, Rais alizungumza kwa muda mfupi sana na
makatibu Muhtasi wa Waziri Mkuu kabla ya kuondoka kuelekea Ikulu,”
ilieleza taarifa fupi ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mapema
wiki hii, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliliambia gazeti
hili kuwa Rais akishakamilisha kazi hiyo ya kuteua Baraza la Mawaziri
waandishi wa habari watajulishwa ili waupashe habari umma wa Watanzania.
Akilihutubia
Bunge na wakati akiwa katika mikutano yake ya kampeni za Uchaguzi Mkuu,
Dk Magufuli aliahidi kuunda Baraza la Mawaziri dogo ikiwa ni mojawapo
ya njia za kudhibiti matumizi ya serikali kwa nia ya kutafuta majawabu
ya kero za wananchi kwa kasi inayostahili.
Na hilo
tayari limeonekana katika hatua kadhaa ambazo amezichukua tangu aingie
Ikulu. Alianza kwa kusitisha safari za nje zisizo na umuhimu mkubwa,
sherehe za Uhuru na kuzipa mwelekeo mwingine kwa mwaka huu na pia
kusitisha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi.
Katika
kipindi kifupi cha uongozi wake, maamuzi mazito kuhusu namna anavyotaka
nchi iende yamefanyika ikiwa na kuhimiza ukusanyaji wa kodi kwa kufanya
ziara ya kushtukiza Hazina na pia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako
alivunja Bodi kabla ya kutumia fedha za sherehe za uzinduzi wa Bunge
(mchapalo) kiasi cha Sh milioni 225 kutumika kuboresha hali ya Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili.
Akiwa
katika kijiji cha Chamwino Ikulu, wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, kasi
yake ya utendaji imeelezwa kuleta maisha mapya katika kijiji hicho.
Kijiji cha Chamwino Ikulu kiliasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu
Julius Nyerere ambako licha ya kuwa na Ikulu Ndogo, upo pia Mnara wa
kumuenzi Rais huyo wa kwanza wa Tanzania.
Mwalimu
Nyerere aliwahi kuishi kijijini hapo kwa miezi mitatu. Aidha, kuna
nyumba zaidi ya 40 zilizojengwa mwaka 1974 eneo la Ntumba baada ya
Mwalimu kuhamasisha wananchi kuwa na makazi bora ambapo wananchi
walifyatua matofali na walikuwa wakikopeshwa na iliyokuwa Benki ya
Nyumba Tanzania (THB).
Pia
Mwalimu Nyerere alipeleka ng’ombe wa maziwa 20, akatengeneza ranchi
yenye ukubwa wa ekari 640 ambayo ilizungushiwa uzio. Ranchi hiyo ipo
eneo la Tairama. Aidha kuna nyumba za kisasa za tembe zilizojengwa kwa
maelekezo ya Mwalimu Nyerere na nyumba za watumishi wa Ikulu, ikiwemo
nyumba ya Mwandishi wa Habari wa Rais na Mwandishi wa Rais ambao nao
waliishi wilaya hiyo wakati Mwalimu akihamasisha uanzishaji wa vijiji
vya ujamaa.
Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma na Mwandishi Wetu, Dar

Post a Comment