Professa Kitila Mkumbo ni mmoja kati ya wasomi ambao ni rafiki wa vyombo vya habari, amekuwa na utii pale anapoitwa katika chombo chochote cha habari na kuzungumzia masuala mbalimbali hasa siasa.
Anapokuwa rafiki wa vyombo vya habari namaanisha pia ni rafaiki wa jamii kwakuwa ni jamii ndiyo inayomsikiliza na kumwona kisha kujifunza kwa mema anayosema.
Niweke wazi tu kuwa ni mmoja kati wasomi ambao huwa nafurahika wanapozungumza kutokana na kuwa muwazi zaidi hata kama jambo analozungumza linapingwa na wengi ili mradi amesimamia ukweli.
Hajali kama anachozungumza kitamkwaza fulani bali anajali kina ukweli kiasi gani.
Siku moja akasema `demokrasia ni hali ya mtu kusikiliza hata kile asichopenda kusikia mara kwa mara`.
Mnaweza kupingana ama kutofautiana katika jambo fulani na ili mpate ufumbuzi lazima mmoja ashindwe kwa hoja na siyo kwa kelele ama kwa sauti yake kuwa juu sana.
Huku katika mchezo wetu wa soka watu kama akina Professa Mkumbo wanahitajika sana na wanahitajika wengi sana ili kwa pamoja tusonge mbele katika soka letu ambalo limezungukwa na uongo mwingi na kupingana bila hoja.
Ukiangalia `Chaguzi` zetu za viongozi wa Soka zimekumbwa na `ombwe` la ulaghai kiasi cha kuongozwa na baadhi ya viongozi wasiyostahili kuongoza soka.
Ukiangalia ndani ya vilabu kadhiya ni hiyohiyo na kadhiya hiyo imesambaa mpaka sasa inaingia katika timu yetu ya Taifa. Ni Hatari.Timu yetu ya Taifa siku kadhaa zilizopita ilitupwa nje ya michuano ya kufuzu ushiriki wa kombe la dunia 2018 kwa kuchapwa jumla ya mabao 9-2 katika michezo yote miwili. Inauma sana.
Inawezekana kipigo cha Stars kisiwe cha kwanza ama cha mwisho na hiyo inategemea sana ni namna gani tumepokea kipigo hicho na tumejisahihisha wapi.
Ni lazima tukae chini na kujadili tulikosea wapi, tupo wapi na tunataka kwenda wapi na kwa muda gani. Kama tutakaa kimya na tusitafute `kisiki` kilichotufanya tujikwae basi tusishangae siku moja Somalia ambayo sasa tunaifunga mabao manne tukaanza kuifunga moja na baadaye sare na kisha tukaanza kupoteza mchezo dhidi yao.
Kama mwaka 2010 tulikuwa tunatoa sare na Algeria nyumbani kwao lakini leo mwaka 2015 tunafungwa saba nyumbani kwao tunaenda mbele au tunarudi nyuma? Mbona maisha yetu ya soka yanakuwa kama hatua za mlevi? Mbili mbele na tatu nyuma.
Yalisemwa mengi kabla ya mchezo huo na baada ya mchezo huo kwa bahati mbaya ama nzuri sikupata fursa ya kuongea chochote baada ya kipigo hicho kilichoniuma sana.
Nimejifunza mengi sana ambayo huenda yakatuletea faida kama wahusika wakuu nao watakuwa wamejifunza kwakuwa naamini ukishajifunza utapata mwangaza kipi kizuri na kipi si kizuri.
Kwa nafasi hii sitoweza kuelezea mengi ama yote niliyojifunza na nitaeleza machache sana kati ya hayo mengi na huenda wewe msomaji unaweza kuwa na somo jingine kama langu ama tofauti lakini yote ni mafunzo na tiba.
Kwanza nimebaini kuwa mchezo wa soka hauna njia ya mkato ili kuyafikia matunda yake.
Kumbe ni kweli kuwa huwezi kuwa na wachezaji watatu wanaocheza soka nje ya nchi yako halafu ukawaondoa nje ya mashindano wapinzani wako wenye wachezaji 18 wanaocheza soka nje ya nchi yao. Na ikitokea hivyo basi huwekwa katika maajabu ya soka!
Pili nimebaini kuwa huwezi kuwa na Ligi `legelege` ambayo huahirishwa mara kwa mara bila sababu za msingi na kisha ukawa na timu bora ya taifa ambayo inaweza kumfunga Algeria nyumbani kwao na nje ya kwao.
Tatu nimejifunza kuwa kuunda kamati ya kusaidia ushindi siku chache kabla ya mchezo si tija kwa ushindi! Na labda inawezekana kufanikiwa ingeundwa mwaka mmoja kabla?
Nne nimejifunza kwamba kupeana maneno ya faraja bila kuangalia uhalisia siyo sababu ya timu yetu kufanikiwa kiuhalisia.
Na Tano na mwisho lakini siyo mwisho kwa umuhimu nimejifunza kuwa na kauli mbiu kwaajili ya mchezo mmoja siyo sababu ya kutupatia ushindi.
Kama alivyosema Proffesa Kitila demokrasia ni hali ya mtu kusikiliza hata yale asiyopenda kuyasikia. Hebu tupeane demokrasia kwa kusikilizana na tuyapatie ufumbuzi matatizo yetu.
Inaumiza sana kuona timu yetu ya Ttaifa inaburuzwa kila kukicha huku sababu tukiifahamu na tunaifumbia macho kwakukusudia ama kwakutokufahamu.
Stars bado inakabiliwa na michezo ya kimataifa hatupaswi kurudi nyuma kwa wakati huu, tupambane kwanza na baada ya matokeo yeyote tuangalie maradhi yetu na tujitibu ili kesho tufurahie.
Post a Comment