0


Mchuano wa kumpata meya wa Manispaa ya Iringa kupitia Chadema umechukua sura mpya baada ya kuahirishwa kwa uchaguzi wa kura za maoni uliokuwa umepangwa kufanyika juzi, kutokana na kuwapo mvutano mkali wa wagombea ndani ya chama hicho.

Kwa mara ya kwanza, Chadema itaongoza baraza la madiwani la manispaa hiyo baada ya kupata viti 21 vya madiwani wakiwamo 14 wa kuchaguliwa, watano wa viti maalumu na wabunge watatu wakiongozwa na Mchungaji Peter Msigwa.

CCM itaingia kwenye baraza hilo ikiwa na madiwani watano, wanne wa kuchaguliwa akiwamo meya aliyemaliza muda wake katika manispaa hiyo, Amani Mwamwindi na diwani mmoja wa viti maalumu.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Iringa, Frank Nyalusi alisema mvutano huo unaonyesha kukua kwa chama.

“Ni kweli kuna mvutano wa nani anatakiwa kuwa meya wa manispaa. Suala hili lipo chini ya viongozi wa kanda,” alisema Nyalusi ambaye pia anawania nafasi hiyo.

Mbali na mwenyekiti huyo kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho, wengine wanaogombea ni katibu mwenezi ambaye ni Diwani wa Kitwiru, Baraka Kimata na Diwani wa Isakalilo, Alex Kimbe.

Kwa upande wa nafasi ya naibu meya, wanaoshindania ni Diwani wa Gangilonga, Dadi Igogo, Diwani wa Kwakilosa, Joseph Lyata na Diwani wa Mkimbizi, Evaristo Mtitu.

Nyalusi alisema japo wameshapatiwa maelekezo ya kupeleka jina la mgombea wa nafasi hiyo manispaa, hajui lini uchaguzi huo utafanyika.

Nyalusi alisema mchakato wa uchukuaji wa fomu za kuomba nafasi hiyo ulianza tangu Novemba 21 na gharama yake ilikuwa Sh50,000 kwa kila moja. Alisema hafahamu lini uchaguzi huo utafanyika baada ya kuahirishwa.

Mratibu wa Chadema, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Frank Mwaisumbe alisema ofisi yake ilitoa agizo la kuahirisha uchaguzi huo ili kupitia sifa za wagombea.

“Nafasi inayowaniwa inahitaji mtu makini, mwenye weledi na uwezo mkubwa wa kufanya kazi za wananchi, hii ni nafasi ya kiserikali siyo ya chama, hivyo lazima tupitie sifa za wagombea ndipo wapigiwe kura,” alisema na kuongeza;

“Kura zinaweza kutupatia matokeo ya kiongozi asiye na sifa, ndiyo maana tumeahirisha uchaguzi ambao tutatangaza tena baada ya mchakato unaotakiwa kumalizika.”

Alisema tayari vikao vya wilaya vya chama hicho vimeshakutana na kupitia sifa za wagombea na watawasilisha mapendekezo yao kwenye kikao cha kanda kabla ya kupeleka Kamati Kuu ya Chadema

Post a Comment

 
Top