Ludewa. Wanachama wa CCM katika Jimbo la
Ludewa mkoani Njombe, leo wanapiga kura za maoni ili kumpata mgombea
ubunge kupitia chama hicho atakayeziba pengo lililoachwa na Deo
Filikunjombe aliyefariki dunia Oktoba 15, mwaka huu.
Makada 10 wa CCM waliochukua na
kurejesha fomu wanatarajiwa kupigiwa kura na wanachama wa CCM ili
kumpata mgombea atakayepambana na wagombea wa vyama vya upinzani.
Makada hao ni Philip Filikunjombe (mdogo
wa Deo Filikunjombe), Edgar Lugome, Johnson Mgimba, Emmanuel Mgaya,
James Mgaya, Jackob Mpangala, Simon Ngatunga, Evaristo Mtitu, Deo
Ngalawa na Zephania Chaula.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Ludewa mjini, Tafuteni Mwasonya
alisema kuwa tayari Mungu amekwishawapatia wananchi wa Ludewa mbunge na
kinachosubiriwa ni taratibu za kidunia zifanyike.
Alisema wananchi wanapaswa kumuomba
Mungu badala ya kusikiliza maneno yasiyo na maana, kwa kuwa anayetakiwa
ni mtu anayeifahamu vizuri Ludewa na mwenye uchu wa kuwaletea maendeleo.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti jana,
baadhi ya wananchi walisema imani na matumaini yao ni kuona wajumbe wa
mkutano wa CCM wanamchagua mtu anayekubalika.
Mmoja wa wakazi hao, Bruno Mtega alisema
wanaamini kuwa mtu atayechaguliwa na wana CCM atakuwa mshindani mzuri
miongoni mwa wagombea ubunge watakaopigiwa kura.
John Haule anayeishi Mavanga mjini hapa,
alisema wagombea wote wana nafasi sawa, lakini yupo mmoja ambaye ni
zaidi ya wote kwa kila kitu.
Alisema licha ya kumpoteza Filikunjombe, wana nafasi ya kuchagua mtu ambaye atafanya vizuri zaidi miaka mitano ijayo.
Post a Comment