KASI ya
Rais John Magufuli imeendelea kutikisa idara na taasisi mbalimbali za
serikali kutokana na mchakamchaka miongoni mwa watendaji na wasimamizi
wanaoendelea kuasa watumishi walio chini yao, kutii falsafa ya ‘Hapa
Kazi Tu’ vinginevyo watajiondoa kwenye mfumo.
Ari ya
uwajibikaji imeonekana kutawala kwenye taasisi mbalimbali za serikali
zikiwemo halmashauri ambako baadhi ya watendaji wameweka bayana kutokuwa
tayari kugeuzwa mbuzi wa kafara kwa kutowajibika kwa watumishi walio
chini yao. Miongoni mwa halmashauri ambazo wakurugenzi wake wamekaririwa
wakisema hawako tayari kuadhibiwa kwa kushindwa kusimamia kasi ya Dk
Magufuli ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini.
Akizungumza
na wakuu wa idara juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,
Sigsbert Kaijage, aliwataka wafanyakazi kuhakikisha wanakwenda na kasi
ya Rais Magufuli chini ya kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ ili kuinua hali ya
maisha ya wananchi na uchumi wa wilaya kwa ujumla. “Mimi sikubali
kugeuzwa mbuzi wa kafara kwa niaba yenu.
Nahitaji
kila mmoja kutekeleza wajibu wake na kama kuna mtu anaona hataki kufanya
kazi katika halmashauri hii kutokana na maslahi, basi ni vizuri
akatafute maeneo mengine, lakini siyo kuendelea kung’ang’ania huku
ukishindwa kuleta tija mahali pa kazi,” alisema Kaijage.
Licha ya
wakuu wa taasisi mbalimbali kuandaa vikao maalumu kwa ajili ya
kuwasilisha maagizo ya rais kwa watumishi walio chini yao, vile vile
katika vikao au hafla zinazowakutanisha na watumishi wa chini yao,
wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kubadilisha mfumo na kuondokana na
kufanya kazi kwa mazoea.
Juzi
kwenye hafla ya kumuaga aliyekuwa Ofisa Tarafa ya Namanyere, Nimrod
Kaishozi ambaye amestaafu kisheria, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mkoani
Rukwa, Idd Kimanta aliendelea kutumia nafasi hiyo kuhimiza umuhimu wa
watumishi kubadilika na kuendana na kasi ya Magufuli.
Kimanta
alisema mtumishi atakayeshindwa kuendana na ‘Hapa ni Kazi Tu’, atafute
mlango wa kutokea haraka iwezekanavyo. Alikiri kuwapo watumishi ambao ni
wagumu kuendana na mabadiliko huku akiwahadharisha dhidi ya kufanya
kazi kwa mazoea. “Falsafa ya Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim
Majaliwa haizungumzwi tu, bali inakwenda kwa vitendo… Ambaye anaona kuwa
hataendana na kasi hiyo, ni bora akaamua kuondoka mapema kabla ya
kuondolewa kazini,” alisema Mkuu wa Wilaya.
Aliwaonya
wanaoendekeza itikadi za kisiasa akisema kitakachofuata ni hatua kali
za kisheria kuchukuliwa dhidi yao vinginevyo, waamue mapema kuacha kazi.
Alisema ameshatoa maelekezo kwa watumishi wote wa Serikali kujipambanua
upya. “Inasikitisha kuona baadhi yao wameendekeza siasa na kuacha mambo
ya msingi ya kuwatumikia wananchi kama ilivyo katika miongozo yao ya
kiutumishi,” alisema.
Akisisitiza
uwajibika, Kimanta aliwaambia kwamba kama ambavyo wengi walimuona ama
kumsikia Dk Magufuli akihutubia Bunge la 11, mambo aliyosema alimaanisha
utekelezaji na uwajibikaji. Alisisitiza kwamba kama yupo mtu anayeona
ni utani, ataanza naye kummaliza.
Naye Mkuu
wa Wilaya ya Arusha, Fadhili Nkulu, alitoa rai kwa wahitimu wa Chuo cha
Uhasibu kilichoko Arusha kutumia taaluma walizopata kwa kuitikia
kaulimbi ya ‘Hapa Kazi Tu’. “Nawasihi mkatumie taaluma yenu vizuri,
sababu serikali tulionayo ‘sasa ni kazi tu’. Atakayeleta mchezo atakuwa
anachezea kibarua chake mwenyewe,” alisema Nkulu aliyekuwa mgeni rasmi
katika mahafali ya 17 ya chuo hicho.
Tangu
Rais Magufuli alipoapishwa Novemba 5 na kuweka wazi msimamo wake kuhusu
uwajibikaji, watumishi serikalini wameendelea kuhadharishwa wakiambiwa
atakayeshindwa kuendana na mabadiliko, yuko kwenye hatari ya kupoteza
kazi. Makatibu wakuu wa wizara mbalimbali wameendelea kukutana na
taasisi zilizo chini yao kueleza maagizo ya rais kwa ajili ya
utekelezaji.
Hotuba
yake bungeni iliyopigilia msumari msimamo wake, imeendelea kuibua
mjadala mkubwa kwenye majukwaa mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii
na vyombo vya habari. Wachangiaji wengi wameasa watendaji wa umma
wanapaswa kutekeleza maagizo ya rais vinginevyo, wapo watakaopoteza
ajira. Wasomi, wanasiasa na viongozi wa sekta mbalimbali binafsi,
wameelezea hotuba yake kuwa ya kihistoria inayoonesha dhamira ya kweli
kwa nchi.
Maeneo
ambayo rais aliyatilia mkazo katika hotuba yake, ni pamoja na ukusanyaji
wa mapato ambao alisema umekuwa chini ya makadirio kutokana na sababu
mbalimbali. Udhibiti wa safari zote za nje ya nchi zisizo za lazima kwa
ajili ya kupunguza matumizi, ni eneo ambalo liliibua mjadala mkubwa
hususani baada ya rais kutoa takwimu za baadhi ya taasisi za serikali
zilizoongoza kwa kutumia fedha nyingi kutokana na safari hizo.
Miongoni
mwa wasomi waliokaririwa na gazeti hili, ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana aliyesema watendaji wa
umma wanapaswa kutekeleza maagizo huku akisema sasa utakuwa mwisho wa
kufanya kazi kwa mazoea. Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe
Zitto (ACT Wazalendo), alisema mtu atakayempinga Magufuli, analinda
mafisadi na ana maslahi nao.

Post a Comment