0

Siri kubwa ya mafanikio mara nyingi ipo kwenye kujifunza hasa kwa wale watu waliofanikiwa zaidi. Ikiwa utaweza kuitumia siri hii, ndani ya muda mfupi utakuwa umeweza kumudu kubadili maisha yako kwa kiasi kikubwa  lakini kama utachukua hatua.

Kwa kulijua hili unalazimka kujifunza kila siku ili kujua mbinu, kanuni na hata hatua wanazotumia matajiri wengi kufanikiwa. Je,  unajua ni kanuni au mbinu zipi zinaweza kukusaidia na kukufikisha kwenye mafanikio. Najua zipo nyingi, lakini kwa leo tuangalie hatua hizi wanazopitia matajiri wengi na kufanikiwa.

1.  Hatua ya kujiwekea vipaumbele.
Ninaweza nikasema hii ndiyo hatua ya kwanza kabisa ya matajiri wote wanayoipitia. Ili kutimiza malengo yao, kitu cha kwanza wanachokifanya ni kuweka vipaumbele. Hata ikitokea wana malengo mengi vipi, lakini kwa kuwa wana vipaumbele inawasaidia kujua ni lengo lipi waanze nalo na lipi waliache.

Vipaumbele ni msingi mkubwa wa maendeleo yoyote yale. Bila vipaumbele hakuna mafanikio yoyote yanayaweza kutokea kwa sababu kila kitu kinakuwa kinafanywa kiholela. Unapoweka vipaumbele inakuwa rahisi kutimiza malengo yako kwa sababu unakuwa unaweka nguvu nyingi za uzingativu sehemu moja na kuleta matokeo mazuri.

2. Hatua ya kutengeneza pesa.
Matajiri walio wengi wana njia nyingi za kutengeneza pesa. Hawa sio watu wa kutegemea njia moja ya kuwaingizia kipato. Na huo ndio ukweli ambao kwa mtu yeyote anayetaka kuwa tajiri anatakiwa kuujua. Ili uwe tajiri lazima uwe na vitega uchumi vingi vya kukuingizia kipato. Hata kama ni kimoja lakini lazima kiwe kimegawanyika sehemu nyingi tofauti.

3. Hatua ya kujifunza kila siku.
Njia nzuri ya kukufikisha kwenye utajiri ni kuangalia matajiri wanafanya nini na kisha na wewe kufanya. Matajiri walio wengi wanalijua hili ndio maana ni watu wa kujifunza kila siku kupitia vitabu na kwa watu waliofanikiwa zaidi yao. Kujifunza ni njia ya uhakika ya kufikia mafanikio kwa haraka, kwa sababu inakuwa rahisi kujua mbinu nyingi za mafanikio kwa muda mfupi.

4. Hatua ya kufanya kitu cha ziada.
Watu wenye mafanikio muda mwingi wanafanya kitu cha ziada cha kuwatoa kwenye hali ya kawaida au kuridhika. Huwa si wepesi sana kuridhika na kujiona kwamba maisha ndiyo wameyaweza, hapana. Ni watu wa kutafuta kitu cha kuwatoa kwenye ‘comfort zone’ zao. Kwa hili hufanikiwa kufikia mafanikio makubwa.

5. Hatua ya kujiwekea malengo ya kifedha.
Ikiwa unataka kupata matokeo unayayapata sasa, endelea kufanya mambo ambayo unayofanya sasa. Hautaweza kubadili maisha yako hata iweje. Huu ndio ukweli halisi, hasa linapokuja suala la kujiwekea malengo ya kifedha. Ili uwe tajiri ni lazima kujiwekea malengo ya kifedha na kubadili kipato chako. Matajiri wengi wanapitia hatua hii muhimu.

6. Hatua ya kutatua matatizo.
Watu wenye mafanikio, mara nyingi wanatatua matatizo. Wanajua kabisa matatizo ndiyo yanayosabbisha wao wawe matajiri. Kama hakuna tatizo maanake inakuwa ni ngumu sana kuweza kufanikiwa. Matatizo yanakuwa yanawapa fursa za kuweza kufanikiwa. Hii pia ni hatua mojawapo muhimu ambayo inapitiwa na matajiri wengi kabla hawajaufikia utajiri huo.

Hizo ndizo hatua za msingi ambazo matajiri wengi wanazipitia. Je, unataka kuwa miongoni mwa mtajiri wa wakubwa kwa baadae? Kama jibu ni ndiyo, ishi na fanya yale wanayofanya matajiri wengi. Njia ya mafanikio itakuwa ni wazi kwako.

Post a Comment

 
Top