Katibu
Mtendaji Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Sheikh Abdulla Talib
Abdulla amesema Taasisi za dini hazipaswi kuegemea upande wa chama
chochote cha siasa ama kushiriki katika kampeni za uchaguzi lakini
zinawajibu wa kujenga jamii ishiriki kikamilifu kufanyika uchaguzi huru
na wa haki na kujenga matumaini makubwa ya kuwa na amani.
Sheikh
Abdulla Talib ameeleza hayo alipokuwa akiwasilisha mada ya nafasi ya
Taasisi za kidini katika kufanikisha uchaguzi wa amani na uadilifu
katika Semina ya kuhamaisha Viongozi wa dini ya Kiislamu kusimamia
amani wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Amesema
dini inamisingi muhimu inayoweza kutumika katika kujenga amani kwani
kuna uhusiano mkubwa wa kinadharia baina ya dini na uchaguzi wa amani na
uadilifu.
Ameongeza
kuwa kufanya kazi ya kujenga amani ni kutekeleza dhamana ya dini kwani
uislamu wakati wote unasisitiza umoja, upendo na amani ya kila mtu.
Katibu
Mtendaji wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana amewaeleza washiriki wa
semina hiyo ambao ni masheikh na wanazuoni kutoka mikoa mitatu ya
Unguja kwamba wanadhima ya kusisitiza kufuatwa sheria na uadilifu
kuanzia sasa mpaka kutangazwa matokeo ya uchaguzi.
“Uchaguzi
wa amani unahitaji kuwepo uadilifu, kufuatwa taratibu na miongozo
katika mchakato wote, ushirikishwaji wa pande zinazohusika kwa mujibu
wa matakwa ya kisheria, kutolewa elimu ya kutosha ya uraia, uwazi na
uwajibikaji pamoja na kuyakubali matokeo,”alieleza Sheikh Abdulla Talib.
Katika
kufanikisha uchaguzi huru na haki Sheikh Talib ameshauri kuwa na
matumizi mazuri ya nyumba za Ibada na maeneo ya kidini pamoja na
matumizi mazuri ya aya, hadithi, nukuu za kihistoria na hekma nyengine.
“Kwa
kuzingatia uhalisia wa uchaguzi, taasisi za kidini zinapaswa kutumia
mbinu na taratibu za kidini na nyenginezo katika kulingania uchaguzi wa
amani, ”aliongeza sheikh Abdulla Talib.
Aliwakumbusha
wanazuoni hao kuwa Zanzibar ni nchi ndogo yenye watu wachache wenye
uhusiano wa karibu na tatizo linapotokea huzigusa familia nyingi hivyo
amewashauri mahubiri yao yalenge kufanyika uchaguzi katika misingi ya
uhuru, uwazi, haki, amani na utulivu.
Washiriki
wa semina hiyo wameiomba Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kuwa waadilifu
na kufuata taratibu na sheria zote za uchaguzi kuanzia hatua za
kuliboresha daftari la wapiga kura hadi kukamilika zoezi la uchaguzi
bila ya kuingiza ushabiki wa kisiasa.
Katika
maazimio yao masheikh hao wametaka kuhakikishiwa usalama wao wakati wa
kutekeleza jukumu la kuwahubiria wafuasi wao kwani wameingiwa na wasi
wasi wa kukamatwa kutokana na visingizio mbali mbali.
Semina
hiyo iliyofanyika katika jengo la Ofisi ya Bima Mperani, iliandaliwa na
Jumuiya ya JUMAZA na UKUEM kwa kushirikiana na mtandao wa kimataifa wa
dini kwa ajili ya kulinda watoto (GNRC)
Post a Comment