5th May 2015
Mwenyekiti wa Chama Wananchi (CUF), Prof. Ibrahim Lipumba.
Prof. Lipumba aliyasema hayo alipokuwa akihutubia kwenye mkutano wa
hadhara na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa)
Alisema ugunduzi wa mafuta na gesi katika mikoa ya Lindi na Mtwara
ni fursa pekee kwa wakazi wa mikoa hiyo kuacha uchumi tegemezi na ni
nafasi ya kubadili hali za maisha.
Aliongeza kuwa uwapo wa badari yenye kina kirefu mkoani Mtwara pia
ni fursa ya kiuchumi, lakini serikali haijatoa kipaumbele kwa wakazi wa
Lindi na Mtwara juu ya rasilimali zilizopo kwenye maeneo hayo, hivyo
kushindwa kuwanuifasha wakazi wake.
Alisema kama Mtwara kitakuwa kituo cha sekta ya gesi, fursa nyingi
za kiuchumi zitafunguka ikiwamo uwapo wa viwanda na vijana wengi katika
mikoa hiyo watapata ajira.
Alisema kuwa inashangaza kuona wakazi wa mikoa hiyo wakikabiliwa na
hali ngumu ya maisha huku wakiwa na rasilimali inayoweza kubadili hali
ya maisha, lakini tatizo kubwa wanalopaswa kutambua ni uongozi uliopo
madarakani kuwa kikwazo cha maendeleo kwa wakazi wa mikoa hiyo.
“Sasa tumieni sanduku la kura kuicharaza CCM na kuiondoa madarakani kwenye uchaguzi ujao,” alisema Prof. Lipumba
Aidha, Prof.Lipumba alisema Tanzania itaendelea kuwa nchi maskini
kutokana na mfumo wa kisiasa uliopo kutokuwa na sheria maalumu ya
kuwawajibisha viongozi wanaotumia fedha za umma vibaya, ambazo kama
zingetumia vizuri nchi ingeweza kuwa na hali mzuri ya kiuchumi.
Alisema wananchi wanatakiwa kuchagua viongozi wenye uadilifu na
wanaojali maslahi ya Taifa, lakini kwa sasa Taifa halina viongozi
waadilifu, ndio maana hata rasilimali zilizopo ni nyingi na
haziwanufaishi wananchi kutokana na nchi kuongozwa na watu wenye
kukumbatia ufisadi.
Aidha Prof.Lipumba aliwataka wakazi wa mikoa hiyo kujitokeza kwa
wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapigakura ili kupata
kitambulisho ambacho itakuwa ni haki ya kuchagua kiongozi wanayompenda
Oktoba, mwaka huu.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment