Katika
siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari na
mitandao mbalimbali ya kijamii kwamba shindano la urembo nchini maarufu
kwa jina la Miss Tanzania limefunguliwa na Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) na kwamba Kampuni ya Lino International Agency LTD ambayo ni
waendeshaji wa shindano hilo imewataka mawakala wake kuanza maandalizi
ya shindano hilo.Taarifa
hizo za kufunguliwa shindano hilo zilienda mbali kwa kueleza kwamba
mawakala wametumiwa kalenda ya mashindano hayo kwa mwaka huu.
Baraza linapenda kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:
1. Wananchi
wapuuze taarifa hizo kwani kusimamishwa kwa shindano la Miss Tanzania
bado kuko palepale kama ilivyoelezwa katika barua ya BASATA ya tarehe
22/12/2014 waliyoandikiwa Lino International Agency LTD ambayo pamoja na
mambo mengine iliwataka warekebishe kasoro kadhaa zilizojitokeza.
Walisimamishwa kwa misimu miwili ya mwaka 2015 na 2016 ili kujipanga
upya na kurekebisha kasoro husika.
2. BASATA
kama msimamizi na mratibu mkuu wa sekta ya Sanaa nchini ndilo
lililolisimamisha shindano hilo baada ya kubaini mapungufu mengi.
Kusimamishwa kwa shindano hili ilikuwa ni kwa njia ya kuufahamisha umma
na kwa maana hiyo kama shindano litafunguliwa njia hiyo-hiyo ya kutoa
taarifa kwa umma itatumika na si vinginevyo.
3. BASATA
linatoa wito kwa Lino International Agency LTD kutumia muda wake mwingi
kufanyia marekebisho mapungufu yaliyojitokeza ili mashindano haya
yatakaporejea yawe na mikakati na hadhi kuliko ilivyo sasa.
4. Aidha,
Baraza linawataka wasanii na wadau wote kuzingatia sheria, kanuni na
taratibu zilizopo katika kuendesha shughuli za Sanaa sambamba na kufuata
mifumo sahihi ya mawasiliano.
Sanaa ni kazi, tuipende na kuithamini
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI
Post a Comment