Dar es Salaam. Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imezitaka kampuni za simu nchini kufuata sheria wanapotaka kufanya mabadiliko ya tozo za huduma zao ili kutoleta mshtuko kwa wateja.
Kauli hiyo imetolewa ikiwa ni siku chache tangu
kampuni za Vodacom, Airtel na Tigo kupandisha bei za vifurushi vya muda
wa maongezi vinavyojumuisha pia ujumbe mfupi na intaneti.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Profesa John Nkoma alisema hayo jana kupitia matangazo yaliyochapishwa katika vyombo vya habari.
Alisema kampuni za simu zinapaswa kutuma
mapendekezo ya mabadiliko ya bei katika mamlaka hiyo kabla ya
kutekeleza bei mpya inayoendana na gharama zao za uendeshaji.
“Kampuni hizo zinapaswa kutoa machaguo kwa kila
kifurushi wanachotoa ili mteja awe na uhuru na kulipia akitakacho,”
alisema na kuongeza. “Wapo wanaotaka kuongea tu. Wengine wanataka kutuma
ujumbe. Na baadhi wanataka intaneti. Kwa kiwango fulani cha fedha
kuwepo na machaguo hayo yote ili kila mmoja alipie kinachomfaa.
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia,
Profesa Makame Mbarawa alisema Serikali inasubiri mapendekezo ya TCRA
kabla ya kufanya uamuzi kuhusu sakata hilo.
“Wao ndiyo wenye mamlaka ya kutoa muongozo na
baada ya kufanya hivyo hutoa ushauri kwetu. Kuanzia Septemba bei
itashuka kwa kuwa ushindani utaongezeka baada ya kampuni ya Viatel
kuanza kutoa huduma. Kwa sasa wanajenga miundombinu...watasambaza
intaneti ya 3G mpaka vijijini,” alisema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, Rene Meza
alikaririwa akisema kuwa ongezeko hilo limesababishwa na ongezeko la
kodi, hivyo walichukua hatua hiyo ili kuepuka hasara.
Post a Comment