Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, Dk Edward Hosea.
Kigoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imekiri kuwapo kwa baadhi ya watumishi wake wanaojihusisha na vitendo vya kupokea rushwa, hivyo kuchafua sifa ya taasisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma
jana, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hoseah alisema tuhuma
zilizotolewa hivi karibuni na taasisi zilizofanya utafiti juu ya masuala
ya rushwa nchini, baadhi yake zina ukweli.
Dk Hoseah alisema wanapokea utafiti huo kama
changamoto na watatumia sheria, kanuni na taratibu kuwapa adhabu
watumishi watakaobainika kujihusisha na vitendo vya rushwa.
“Takukuru siyo malaika, iwapo nitasema hakuna
kabisa rushwa ndani ya taasisi hii nitakuwa ninajidanganya kwani hili
tatizo lipo sehemu zote, inawezekana maofisa wasio waadilifu wanapokea
rushwa lakini ninawahakikishia kwamba tutachukua hatua kali dhidi ya
yeyote atakayebainika,” alisema Dk Hoseah na kuongeza:
“Serikali imefanya jitihada kubwa kuhakikisha Takukuru inaboreshwa, ndiyo maana bado sielewi kwanini kuna baadhi ya watumishi wanalalamikiwa kujihusisha na ulaji rushwa, wanalipwa vizuri na kuna mazingira mazuri ya kufanya kazi. Nitafanya jitihada kuondoa changamoto hizi.”
Pia, alitoa tahadhari kwa wananchi kuwa makini na
matapeli wanaojitangaza kwamba wao ni maofisa wa Takukuru, hivyo kuomba
rushwa kwa baadhi ya maofisa wa Serikali na watu wengine ambao
wanabainika kufanya makosa yanayohusiana na ubadhirifu mbalimbali.
Dk Hoseah alisema ili kupambana na rushwa lazima
Serikali iwe na uongozi bora na imara, ambao utasaidia kuweka mipango
thabiti kwa maendeleo ya wananchi, kufanya mambo kwa uwazi, kuwajibika
kwa umma, kuwashirikisha watu katika mipango mbalimbali na kusimamia
utawala wa kisheria.
Post a Comment