Prof. Muhongo
Juzi Profesa Sosperter Muhongo alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Nishati na Madini, akieleza kuwa anataka nchi isonge mbele kwa kuwa suala la kumtaka Rais amwondoe kutokana na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, limesababisha mambo mengi kukwama.
Profesa Muhongo amekuwa waziri wa pili kuondoka
baada ya Profesa Anna Tibaijuka kuvuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kutokana na kuingiziwa kwenye akaunti yake Sh1.6
bilioni na mmiliki wa zamani wa IPTL, fedha ambazo zinahusishwa na
sakata la escrow.
Mbali na mawaziri hao, tayari Jaji Fredrick Werema
amejiuzulu kazi yake ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, akieleza kuwa
ushauri wake kuhusu fedha za escrow haukueleweka na kusababisha tafrani.
Pia, katibu mkuu wa wizara hiyo, Eliackim Maswi
amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa sakata hilo, wakati watumishi
watano wa Tanesco, Benki Kuu (BoT) na Mamlaka ya Mapato (TRA)
wamefikishwa mahakamani wakishtakiwa kwa kupokea rushwa inayohusu sakata
hilo. Kashfa hii ni moja ya matukio mengi makubwa yaliyosababisha Rais
kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri. Baadhi ya matukio hayo ni
kashfa ya Richmond, CAG na Operesheni Tokomeza ambazo zilisababisha Rais
kupangua baraza lake.
Ni jambo la kupongeza kwamba angalau hatua
zimechukuliwa kwa kiwango fulani katika kushughulikia tatizo hilo
lililohusu uchotwaji wa takriban Sh306 bilioni kutoka kwenye akaunti
hiyo iliyokuwa BoT.
Kitu cha ajabu ni hii tabia inayoendelea kujengeka
ya kuibuka kwa kashfa, mawaziri kujiuzulu, kuundwa kwa baraza jipya na
baadaye mambo kuendelea kama kawaida kusubiri kashfa nyingine kuibuka
bila ya hatu za dhati kuchukuliwa kudhibiti matukio kama hayo.
Jambo la ajabu ni kwamba kila kashfa inapoibuka,
hutumika nguvu nyingi kuizua au kutetea viongozi wa Serikali hadi mambo
yanapoonekana kuwa yamekuwa makubwa ndipo hatua zichukuliwe.
Tumeona katika kashfa ya escrow zilitumika nguvu
nyingi kutetea wahusika hadi maji yalipozidi unga ndipo hatua
zilipochukuliwa na kushughulikia wahusika. Kitu kibaya ni kwamba hadi
wakati hatua zinaanza kuchukuliwa, tayari Serikali inakuwa imeshafuka na
wananchi wameshaumia.
Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri sasa yamekuwa ya
kawaida kwa kuwa kila yanapofanyika hazichukuliwi hatua thabiti kuzuia
kashfa zisitokee. Suala la fedha kuchotwa kwa fedha zinazokuwa BoT sasa
linaonekana kuwa la kawaida kwa kuwa kashfa ya Akaunti ya Malipo ya
Madeni ya Nje lilipotokea, hakukuchukuliwa hatua madhubuti kuziba mianya
kama hiyo kwenye taasisi hiyo nyeti ya fedha.
Tunadhani ni wakati mwafaka sasa kwa Serikali
kuweka misingi imara ya uongozi itakayowabana viongozi wetu kujiingiza
kwenye kashfa kama hizo. Misingi hiyo pia ihusishe hatua kali ambazo
zinaweza kuchukuliwa kwa viongozi ambao wataingia kwenye kashfa hizo kwa
makusudi au uzembe ili kuzuia wengine kufanya mambo ya aibu na
yanayoumiza wananchi.
Pia, siyo ufahari kuwawajibisha viongozi wakati
ufisadi umeshafanyika kama ilivyokuwa kwenye sakata la EPA na sasa
escrow kwa kuwa fedha za walipa kodi zinakuwa zimeshachotwa. Ufisadi
unatakiwa uzuiwe mapema kuliepusha Taifa kupoteza mabilioni ya fedha na
wanaowajibishwa wachukuliwe hatua kwa kujaribu kula njama za ufisadi na
siyo kuadhibiwa kwa kufanya ufisadi.
Kadri Serikali inavyoonekana kuweka mikakati ya
kuwakingia kifua watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, ndivyo vitendo hivyo
vinavyozidi. Serikali inatakiwa ionyeshe kuchukia ufisadi kwanza.Na ikichukia ufisadi, basi kujiuzulu wa kuwavua madaraka wahusika
kutakuwa ni moja ya hatua za kuwashughulikia wahusika wote nah ii
itasaidia kupunguza vitendo hivyo.MWANANCHI
Post a Comment