Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania linapenda kutoa taarifa kwa wananchi na
Vyombo vya Habari kuhusu mgogoro wa eneo la TONDORONI lililopo katika
Wilaya ya Kisarawe kama ilivyokaririwa na baadhi ya Vyombo vya Habari
hapa nchini.
Taarifa
zilizotolewa na kukaririwa na baadhi ya Vyombo vya Habari kwamba
Wanajeshi wametumia nguvu kuwatoa wananchi eneo la TONDORONI na baadhi
yao kudai kupotelewa na mali zao siyo za kweli na ni za kuwapotosha
wananchi kwa sababu wananchi hao walitaarifiwa kuondoka kupitia uongozi
wa Wilaya na uongozi wa Vijiji vya MLOGANZILA na KILUVYA B. Aidha,
walipewa muda wa kutoa vitu vyao na wao kuondoka.
JWTZ
linapenda kuwahakikishia wananchi kuwa hatua ya kuwaondoa wananchi
wavamizi kutoka katika eneo la kambi ya Jeshi kwa uangalifu, umakini na
kulikuwa na usimamizi wa hali ya juu na hakuna mali ya mwananchi
iliyoporwa kama ilivyodaiwa. Ifahamike kwamba; Jeshi linaona ni bora
lilaumiwe kwa kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo hatarishi ya jeshi
ambayo hutumika katika mafunzo yanayohusisha risasi za moto, zana hatari
za kijeshi na mabomu ambayo wakati mwingine hulipuka baada ya muda
fulani kupita badala ya kuwaacha wakae katika maeneo hayo kutokana na
sababu za kisiasa au ushabiki mwingineo na hivyo kuwa katika hatari ya
kuweza kuumia vibaya au kupoteza maisha yao na mali zao.
Pia ni vema tukajua historia ya tatizo hili.
Mnamo
mwaka 1978 eneo linalojumuisha vijiji vya MLOGANZILA na KILUVYA B na
kilichokuwa kijiji cha TONDORONI lilichukuliwa na Serikali kwa ajili ya
matumizi ya JWTZ. Baada ya maamuzi hayo Kikosi cha JWTZ kilihamia
TONDORONI mwaka 1981na kukalia eneo la hekta 4197. Serikali ililipima
eneo la TONDORONI kisheria mwaka 1984 na eneo lote liliwekewa mawe ya
mipaka.
Baada ya
hapo, Serikali ilifanya tathimini ya malipo kwa awamu mbili. Awamu ya
kwanza ilikuwa mwaka 1987/88 na wakati huo kulikuwa na wananchi wapatao
1,508. Awamu ya pili ilifanyika 1992/93 ambayo ilijumuisha tathmini ya
nyumba na majengo ambapo wananchi wengine 955 walifanyiwa tathimini.
Kufuatia tathimini iliyofanyika malipo yalikuwa kama ifuatavyo:
Mwaka 1996 malipo yalifanyika kwa barua kumbukumbu Na. FE 98/371/01/73 ya tarehe 11 Juni 2003.
Malipo
mengine yalifanyika mwaka 2002 na 2006. Baada ya Malipo hayo, mengine
tena yalifanyika mwaka 2012 kutokana na kesi ya madai Na. 144/1996. Kwa
hiyo madai ya msingi ya wananchi yalishalipwa na sheria ya uchukuaji
ardhi imetekelezwa kikamilifu.
Hata
hivyo, mwaka 2005 baadhi ya wananchi wachache walifungua kesi Na.
78/2005 ambayo baadae ilifutwa na mahakama. Tarehe 10 Dec 2013 M/kiti wa
kamati ya Ulinzi ya Wilaya Kisarawe alikwenda eneo la TONDORONI
kuwasomea wananchi maamuzi ya mahakama akiandamana na mwanasheria wa
Wilaya ya Kisarawe.
Pamoja na
taarifa hizo kupitia uongozi wa Wilaya na uongozi wa Vijiji vya
MLOGANZILA na KILUVYA B. wananchi wachache wameendelea na kazi
zinazochangia kuharibu mazingira hasa ukataji wa miti, uchomaji wa mkaa
na kuwasha moto mara kwa mara hali inayotishia usalama wa kambi na wa
wananchi wenyewe ikizingatiwa kwamba hili ni eneo la mafunzo ambapo
risasi za moto hutumika sambamba na zana zingine hatari za kijeshi
katika eneo hilo.
Wananchi
waliowengi wanajua ukweli kuwa eneo la TONDORONI linamilikiwa kihalali
na JWTZ, lakini wapo wananchi wachache wamekuwa wakiingia kinyemela
katika eneo hilo na kufanya ujenzi mpya usiku licha ya jitihada
mbalimbali zinazofanyika kuwaelimisha na kuwashauri kuwa waache tabia
hiyo ya kulivamia eneo hilo la Jeshi, jambo ambalo hugunduliwa na
kuzuiliwa uendelezaji wa ujenzi huo.
Jeshi
linawataka wananchi wachache wanaovamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya
matumizi ya kijeshi; kutambua kuwa kufanya hivyo ni kosa la kisheria
lakini pia kwa mara nyingine tena kuendelea kuwakumbusha wananchi kuhusu
madhara yanayoweza kuwapata wananchi wanaovamia maeneo ya Jeshi na
kujenga katika maeneo hayo.
Jeshi
litaendelea kushirikiana na wananchi wema na kuheshimu mipaka iliyopo
baina ya makambi yake na maeneo ya wananchi lakini pia litaendelea
kuwaondoa wale wachache wanaojenga katika maeneo yake kinyume cha
utaratibu.
Imetolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano
Makao Makuu ya Jeshi, Upanga
Post a Comment