James Mbatia |
Dar es Salaam. Chama
cha NCCR-Magezi kimesema, vigogo wote waliohusika kutoa na kupokea
mgawo wa fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow wafikishwe mahakamani
akiwamo Mkurugenzi wa VIP Engineering Ltd, James Rugemalira .
Kashfa hiyo imesababisha Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko madogo
ya baraza lake la Mawaziri kutokana na mawaziri wawili kujiuzulu.
Mawaziri waliotajwa kwenye sakata hilo ni Profesa Anna Tibaijuka, ambaye
alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na aliyeingiziwa
Sh1.6 bilioni na mwanahisa wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James
Rugemarila.
Wengine waliopata mgao huo kutoka kwa Rugemarila na kiasi katika mabano
ni Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge (Sh1.6 bilioni),
Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja (Sh40.4 milioni), aliyewahi
kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4 milioni), Mbunge
wa zamani wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh40.4 milioni) na aliyekuwa
mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni).
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena
Nyambabe alisema waliofikishwa mahakamani hadi sasa ni vidagaa lakini na
vigogo mashuhuri wakiendelea kutamba.
“Mpokeaji na mtoaji wa rushwa wote ni wahalifu na wanatakiwa kufikishwa
mbele ya mahakama ili wajibu tuhuma zinazowakabili...Rugenarila naye ni
miongoni mwa watu wanaotakiwa kufikishwa mahakamani.”
“NCCR tunataka kujua kwa nini baadhi waliopewa rushwa wamefikishwa
mahakamani lakini watu wengine kama Profesa Tibaijuka, Chenge, Ngeleja,
Yona, Kimiti na wengineo hawafikishwi mahakamani? Wote wanatakiwa kwenda
kujibu tuhuma zao,” alisema Nyambabe
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk
Edward Hoseah alipotafutwa kuzungumzia kauli hiyo ya NCCR alisema, “Sipo
ofisini hivyo nisingependa kulizungumzia hilo.”
Waliofikishwa mahakamani hadi sasa ni Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Umeme
Vijijini (Rea), Theophillo Bwakea na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma,
ambao kwa pamoja wanadaiwa kupokea rushwa ya Sh485.1 milioni.
Wengine ni Meneja Misamaha ya Kodi wa TRA, Kyabukoba Leonard Mutabingwa,
Mwanasheria Mwandamizi wa Tanesco, Steven Roman Urassa na Mkurugenzi wa
Fedha BoT, Julius Rutta Angello wanaokabiliwa na mashtaka ya kuomba na
kupokea rushwa ya jumla ya Sh1.923 bilioni.
Post a Comment