Muonekano
wa lori lenye namba za usajili T122 ALW baada ya kugongana na basi la
Fanuel Express yenye namba za usajili T919 DCD katika Kijiji cha
Ibetelo eneo la Nyororo, wilayani Mufindi mkoani Iringa.
ZAIDI ya
watu 4 wamefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya basi la
abiria kutoka Mbeya kwenda Dodoma kugongana na lori katika Kijiji cha
Ibetelo eneo la Nyororo wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Kamanda
wa Polisi Mkoani Iringa, Ramadhani Mungi amesema kuwa ajali hiyo
imetokea saa 4.45 asubuhi na kuhusisha basi mali ya Kampuni ya Fanuel
Express yenye namba za usajili T919 DCD kugongana uso kwa uso na lori
lenye namba za usajili T122 ALW mali ya Kampuni ya Transisco lililokuwa
likitokea Dar es Salaam kwenda nchi jirani.
Amesema
watu wawili waliokuwa ndani ya basi wamefariki papo hapo na wote
waliokuwa ndani ya lori wanahofiwa kufa, ambapo hadi kufikia saa 7
mchana, watu wawili ndani ya lori walikuwa wamethibitika kufariki dunia
na kufanya waliokufa kuwa wanne.
Zoezi la kuondoa miili iliyokuwa ndani ya lori linaendelea ambapo amesema kuwa huenda idadi hiyo ya waliokufa ikaongezeka.
Akielezea
mazingira ya ajali hiyo, Kamanda Mungi amesema kuwa basi hilo lilikuwa
likijaribu kulipita basi lililokuwa mbele yake katika eneo ambapo
palikuwa na lori lingine lililoharibika, wakati huo huo lori
lililohusika katika ajali hiyo lilikuwa likikwepa lori lililoharibika
pamoja na basi hilo, ndipo magari hayo yalipogongana uso kwa uso katika
jitihada za kukwepana.
Majeruhi wa ajali hiyo wamepelekwa katika Hospitali ya Mafinga, Iringa
Post a Comment