0

Licha ya miaka mingi Mtwara kusifika kwa korosho, uzalishaji wa zao hilo sasa unaporomoka kila kukicha.
Imeelezwa kuwa katika msimu wa mwaka 2013/14, zao la korosho lilikuwa la pili kwa kuingiza fedha za kigeni nchini, huku zao la tumbaku likishika nafasi ya kwanza.
Hata hivyo, pamoja na zao hili kuwa muhimu kwa pato la Taifa, bado halijaweza kumkomboa mkulima kiuchumi, hali inayowafanya kuzidi kudidimia.
Watalaamu wamekuwa wakieleza kuwa hali hiyo inatokona na uzalishaji kuwa mdogo.
Uzalishaji huo mdogo unatokana na miti ya zao hilo kwua chini ya viwango, hivyo kusababisha kupanda kwa gharama za uzalishaji.
Baadhi ya wakulima walisema kuwa ipo haja kwa Serikali kuingilia kati kuwasaidia ili kilimo hicho kiboreshwe na kuleta faida zaidi kwa nchi na pato la mtu binafsi kwa maana ya mkulima.
Upendo Millanzi, mkulima kutoka Kijiji cha Naliendele, Wilaya ya Mtwara anasema zao hilo limeshuka kutokana na kukosa pembejeo.
Kadhalika, mabadiliko ya hali ya hewa yamechangia kwa kiasi kikubwa zao hilo kushindwa kustawi.
“Kusema kweli zao la korosho limeshuka sana, hii ni kwa sababu mbalimbali zikiwamo ukosefu wa pembejeo na kama zinapatikana basi siyo kwa wakati husika, hivyo kushindwa kumsaidia mkulima kuendelea kufanya kazi za uzalishaji,” anasema Millanzi na kuongeza kuwa.
Aliongeza: “Inashangaza sana mkulima anakwenda kwenye chama cha ushiriki kufuata pembejeo, anaambiwa zimekwisha, lakini hujui ni nani aliyechukua.
Anasema kuwa, pembejeo hizohizo zinauzwa kwa wafanyabiashara kwa bei ya juu ambayo mkulima wa kawaida hawezi kumudu.
Kwa upande wake, mkulima Hassan Mkichana anaeleza sababu nyingine inayofanya zao la korosho kushuka ni kutokana na miti kukaa muda mrefu, hivyo kushindwa kutengeneza ubora na kuwataka wananchi kuachana na kilimo cha miti ya zamani.
“Baadhi ya mikorosho inaonekana kuzaa vizuri na kuwa na mazao bora kutokana na mkulima kutumia miche ya kisasa iliyothibitishwa na wataalamu wa kilimo cha zao hilo.
Ili kufikia malengo ya uzalishaji bora wa zao la korosho, wakulima wanapaswa kununua miche ya kisasa na kuachana na ile ya zamani ambayo haijali mvua wala pembejeo.
“Wanaoipata hii miche ni wale wenye uwezo kifedha, hivyo tunaiomba Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ipunguze bei ili wakulima wengi wapate nafasi ya kununua.
Ni vizuri kwa Serikali kupitia wizara husika kufuatilia matatizo ya wakulima wa zao la korosho.
Kwa Upande wake mama Sijaona, mkulima wa zao la korosho Kata ya Naliendele, anasema sababu za kushuka kwa zao la korosho ni pamoja na upandaji wa miche ya mikorosho ya zamani, hali inayochangia zao hilo kushuka thamani tofauti na mikorosho ya kisasa ambayo imefanyiwa utafiti na wataalamu.
“Sababu zingine za kushuka kwa uzalishaji wa korosho kwa Mkoa wa Mtwara ni utegemeaji wa mikorosho ya zamani,” anasema Sijaona.
Anaitaja sababu nyingine kuwa ni kutozingatia yale yanayotolewa na wataalamu kuhusiana na dawa, kwani wapo baadhi ya wakulima wamekuwa wakipotoshwa kutumia dawa za mazao mengine katika mashamba ya korosho na kusababisha zao hilo kudidimia ikiwa ni pamoja na tatizo la ucheleweshwaji wa pembejeo.
“Aidha baadhi hawazingatii yale yanayoelezwa na wataalamu. Kwa mfano, mkulima anaambiwa atumie dawa fulani kwa vile inafaa kwenye zao la korosho, lakini yeye anatuacha na kutumia dawa isiyo sahihi hivyo kuleta madhara,” anasema na kuongeza:
“Wakati wa kupulizia korosho unapofikia, pembejeo zinakuwa bado hazijafika, kwa hiyo awamu ya kwanza ya kupuliza haiwezi kumaliza tatizo bila ya awamu ya pili kufanyika,” anasema na kuongeza:
“Hali hii imekuwa ikichangia uzalishaji kupungua. Ombi letu kwa Serikali, itusaidie pembejeo kwa wakati wake. Pia elimu itolewe kwa ubora zaidi, ili wakulima waelewa na kuzingatia,” anasema Kijacho.
Mtaalamu wa masuala ya kilimo, Dk Louis Kasuga, ambaye pia ni Mtafiti mwandamizi wa Kituo cha Utafiti cha Naliendele, Mtwara anasema kilimo cha korosho ni moja ya zao la biashara na kuna umuhimu wa kuhakikisha wakulima wanabadilika.
Anasema iwe ni kwa kilimo chochote, ni lazima kanuni za kilimo bora zizingatiwe ili kuhakikisha mkulima ananufaika na kilimo na kumletea tija.
Dk Kasuga anasema kutokana na misingi hiyo, kuna kila sababu za kuhakikisha taaluma mbalimbali zinahamasishwa kusaidia kukuza mfumo mzima wa ukuaji wa kilimo cha korosho.
Dk Kasuga pia anaeleza kuwa hata wakulima nao wanatakiwa kubadilika na kuona kuwa taaluma zilizobuniwa na watafiti zinazingatiwa.
Akatolea mfano wa utafiti ambao unaonyesha kuwa kilimo cha mikorosho ya zamani kinapaswa kutotiliwa kipaumbele, badala yake wakulima wazingatie kilimo cha kisasa.
“Wakulima waelewe kuwa mikorosho mingi waliyonayo ni ya zamani, inatoa korosho kidogo, hivyo ni lazima wabadilike kwa kuwa na mikorosho ya kisasa. Mikorosho ya kisasa haishambuliwi sana na wadudu kama ilivyo mikorosho ya zamana,” anasema Kasuga.
Anaongeza: “Kama wakiweza kupokea vizuri na kufanyia kazi ushauri wa wataalamu, wakulima watakuwa na mafanikio makubwa.”
Msomi hiyo anabainisha kuwa kuna mashamba ya kuzalisha mbegu za mikorosho kwa ajili ya wakulima.
Mashamba hayo yako Mkoa wa Tanga na Pwani katika maeneo ya Naliendele, Nanyanga wilayani Tandahimba, Mtopwa –Newala, Nyangao- Lindi,Mkumba –Nachingwea na Nakayaya wilayani Tunduru.MWANANCHI

Post a Comment

 
Top