Mtu
mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika mapigano
katika mji wa Mombasa pwani ya Kenya. Polisi walipambana na vijana
walioingia katika Msikiti wa Swafaa eneo la Kisauni na mpaka sasa zaidi
ya vijana 400 wanashikiliwa tangu kuanza kwa msako huo, mapema wiki hii.
Mwandishi
wa BBC, Emmanuel Igunza anasema Msikiti huo ulifungwa jana baada ya
polisi kuuvamia Jumatano, ambamo walipata magruneti, mabomu ya petroli
na silaha nyingine. Hali ya wasi wasi bado imetanda katika mji huo wa
pwani. Serikali imekwishafunga misikiti minne ambayo wanasema ina
uhusiano wa watu wenye misimamo mikali ya imani ya kidini.Awali polisi mjini Mombasa pwani ya Kenya walisema wamepata silaha nyingine zaidi yakiwemo mabomu katika msikiti wa tatu ambao ulifanyiwa upekuzi
Msako huo katika msikiti wa Swafaa mtaani Kisauni unakuja baada ya msako mwingine wa Jumatatu ambapo polisi pia walipata silaha ndani ya msikiti ambao wanasema hutumika kutoa mafunzo yenye itikadi kali.
Mtaa wa Kisauni ndiko vijana waliokuwa wamejihami kuwadunga visu watu wanne na kuwaua. Pia waliwashambulia kwa silaha nyingine.
Waziri wa usalama wa ndani, Joseph Ole Lenku anasema kuwa msako huo ulifanywa katika misikiti ambayo hutumiwa na watu wanaoeneza itikadi kali za kiisilamu kwa vijana ambao inadaiwa wanajiunga na kundi la wapiganaji wa kiisilamu la Al Shabaab nchini Somalia.
Viongozi wa kiisilamu wamelaani misako hiyo katika Misikiti wakisema kuwa itachochea zaidi vijana kuendeleza itikadi kali za kidini.
Post a Comment