Maandamano ya walimu kuingia katika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba
kuadhimisha Siku ya Walimu Duniani, jana yalipata mtafaruku baada ya
polisi kuyaingilia na kuchana bango mojawapo lililohoji posho za wajumbe
wa Bunge la Katiba.
Bango hilo la kitambaa cheupe lilikuwa na maandishi yanayohoji posho
ya Sh300,000 waliyokuwa wanapata wajumbe wa Bunge la Katiba,
yakilinganishwa na kazi kubwa wanayofanya walimu.
Ujumbe wenyewe ulisomeka hivi: “Haki iko wapi usawa uko wapi, posho
ya mjumbe wa Bunge la Katiba kwa siku shilingi laki tatu, mshahara wa
mwalimu shilingi 370 kwa mwezi. No big results without big salary
(Hakuna matokeo makubwa bila mshahara mkubwa)”.
Ujumbe huo ulikuwa ukifanya rejea ya viwango vya malipo ya Sh300,000
kwa siku ambazo walikuwa wakilipwa wajumbe wa Bunge Maalumu zikiwa ni
Sh230,000 kama posho ya kujikimu na Sh70,000 ambazo ni posho ya vikao.
Hata hivyo bango hilo lilichanwa hatua chache kabla ya walimu hao
hawajaingia uwanjani humo, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda.
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), mkoani Kagera Dauda
Bilikesi, alisema amesikia habari za bango hilo kuharibiwa lakini
akasema asingezungumza kwa kina kuhusu suala hilo kwa kuwa hayo
yamepita.
Waibuka na shairi
Muda mfupi baada ya polisi kuharibu bango hilo lisionekane uwanjani,
walimu hao walipiga chenga kiana wakaibuka na ujumbe ule ule kwa njia ya
shairi.
Kupitia shairi hilo liliposomwa mbele ya Pinda, walimu walihoji
ukubwa wa posho za wajumbe wa Bunge la Katiba zikilinganishwa na
mshahara wanaopata, hali iliyosababisha umati wa walimu uliokuwa
uwanjani hapo kulipuka kwa sauti kubwa za shangwe.
Shairi hilo lililosomwa na Mwalimu Betwel Magoso kutoka Wilaya ya
Biharamulo, lilisababisha kuvurugika kwa muda kwa utaratibu uliopangwa
kwa mujibu wa ratiba, pale alipohoji wajumbe wa Bunge la Katiba kupata
Sh1 milioni kwa siku tatu ambazo ni mkopo wa mwalimu kwa miaka mitatu.
Mwalimu Magoso alimgusa Pinda ambaye kabla ya kuanza hotuba yake
alianza kwa kusema kuwa mwalimu huyo alitumia ujanja kufikisha ujumbe
wake na kuwa baadhi ya maneno katika shairi lake yalikuwa ni mazito.
Kanuni za mafao zasitishwa
Katika hatua nyingine, Serikali imesitisha matumizi ya kanuni mpya za
ukokotoaji mafao ya pensheni ambao umeibua malalamiko kuwa malipo ya
mkupuo yalipunguzwa kutoka asilimia hamsini hadi ishirini na tano.
Kanuni hizo ni zile zilizotungwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii (SSRA) na kutangazwa Agosti 6, mwaka huu mjini Dodoma
na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka.
Tangu kutangazwa kwake kanuni hizo zilizua malalamiko kutoka kwa
wadau mbalimbali hususan wafanyakazi ambao walisema kuwa hayalengi
kuboresha wala kuhuisha mafao, bali yanapunguza stahili hiyo tofauti na
ilivyokuwa mwanzo.
Akihutubia sherehe hizo, Pinda alisema suala hilo linarejeshwa tena serikalini kuangaliwa upya.
“Acha suala hili tulirejeshe serikalini tukalitazame upya kwa sababu
halikubaliki na hatuwezi kulishurutisha kwa sababu nyie ndiyo wadau,
siyo sisi. Tutawaambia walitazame tena na warudi wawashirikishe vizuri
wawaeleze mlikubali au mlikatae,” alisema Pinda.
Waziri Mkuu alisema pamoja na kuwa lengo lilikuwa ni kuboresha maisha
ya wafanyakazi kwa kuleta mfumo mpya wa ukokotoaji wa mafao ya
pensheni, suala hilo lilihitaji ushirikishwaji mpana zaidi ikiwa ni
pamoja na wadau wenyewe.
Katika kuunga mkono kilio cha walimu, Pinda alitoa mfano wa wabunge
wanaopata mafao yao yote wanapomaliza kipindi cha uwakilishi kwa miaka
mitano na kuwa kabla ya hapo mafao hayo yalitolewa baada ya kumaliza
miaka kumi, jambo ambalo halikupendelewa na wabunge.
Kauli hiyo ilitokana na risala ya walimu iliyosomwa na Katibu Mkuu wa
CWT, Yahya Msulwa aliyesema mabadiliko hayo yamezua manung’uniko
makubwa hasa kwa walimu wanaobeba idadi kubwa ya watumishi.
Alisema mfumo wa ukokotoaji wa mafao wa zamani, pamoja na kuwa
mishahara yao ni midogo, ulifanya mafao yao ya uzeeni yawe na unafuu kwa
kiwango fulani, ikilinganishwa na mfumo mpya ambao ukokotoaji
unafanyika kwa kuangalia wastani wa mishahara ya miaka mitatu ya mwisho.
Kabla ya mapendekezo hayo, ukokotoaji wa mafao ulifanyika kwa
kuangalia mshahara wa mwisho wa mtumishi na malipo yalitolewa kwa
asilimia hamsini ya mafao yote baada ya ukokotoaji kufanyika.
Na Phinias Bashaya, Mwananchi
Post a Comment