Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa
(Necta) limetangaza kuanza kutoa vyeti mbadala kwa gharama ya Sh100,000
kwa wote ambao vyeti vyao vimeharibika kiasi cha kutofaa kwa matumzi.
Tangazo hilo lililotolewa jana na Necta,
linawalenga wote waliohitimu elimu zao kuanzia Oktoba 2008, ambao vyeti
vyao vina picha za watahiniwa husika, huku likifafanua kuwa waliomaliza
kabla ya hapo, utaratibu wa kuwatumia uthibitisho wa matokeo katika
taasisi zenye mahitaji utaendelea.
Kwa mujibu wa tangazo hilo: “Ombi la cheti mbadala
litapokewa baada ya miezi mitatu kupita tangu upotevu wa cheti halisi
kutangazwa gazetini.
Uchunguzi wa uthibitisho utafanyika kwa siku 30
tangu kupokewa kwa ombi la cheti mbadala kwa kuihusisha polisi (kitengo
cha uchunguzi wa picha).”
Katika kukabiliana na udanganyifu unaoweza
kujitokeza kutoka kwa watu wasio waaminifu, baraza hilo lilisema kuwa
hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaoshiriki katika
uombaji wa vyeti hivyo vitakavyokuwa na neno ‘duplicate’ ili
kuvitofautisha na vyeti halisi.
“Cheti mbadala kitatolewa mara moja tu na endapo
itabainika kuwa cheti halisi bado kinatumika katika soko la ajira au
mafunzo na mtahiniwa akathibitika kushiriki katika kuidanganya Necta,
hatua kali za kisheria zitachukuliwa,” inaonya fomu ya maombi ya cheti.
Waliopoteza vyeti halisi watatakiwa kutoa taarifa
polisi na kutangaza gazetini, huku waliounguliwa au vyeti vyao
kuharibiwa na mchwa, mafuriko, panya au kwa namna nyingine yoyote
watatakiwa kuwasilisha vielelezo husika pamoja na barua ya Serikali ya
Mtaa wa eneo la tukio la moto au mafuriko yalipotokea.
Taarifa hiyo ilisema kuwa, iwapo yapo mabaki ya cheti husika, watatakiwa kuyawasilisha Necta.
Tangazo la gazetini la upotevu wa cheti litatakiwa
kuwa na taarifa muhimu kama jina la mtahiniwa, namba ya mtihani, aina
ya mtihani, mwaka wa mtihani, jina la shule na picha ya mtahiniwa.
Baada ya polisi kutoa hati ya upotevu wa cheti,
mwombaji atatakiwa kuambatanisha picha ndogo mbili pamoja na nakala ya
kitambulisho na risiti halisi ya malipo.
Pia, katika mwendelezo wa kujiridhisha kuwa kila
mtumishi au mwanafunzi anakuwa na cheti chake baada ya taasisi
mbalimbali pamoja na idara za Serikali kuanzisha utaratibu wa kuhakiki
taarifa za kitaaluma hasa vyeti vinavyotolewa na baraza hilo.MWANANCHI
Post a Comment