Dodoma. Wiki ya kufa au kupona kwa Bunge la
Katiba, inaanza leo mjini Dodoma wakati wajumbe watakapoanza kuzipigia
kura ibara na sura za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.
Shughuli hiyo itaanza huku kukiwa na hofu ya
kutopatikana kwa theluthi mbili ya kura kwa wajumbe kutoka Tanzania Bara
na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar inayotakiwa kwa mujibu wa
kanuni, sheria na Katiba ya nchi.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa wiki iliyopita
na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, upigaji kura utafanyika
kwa siku nne kuanzia leo hadi Oktoba 2, mwaka huu na iwapo itapitishwa,
atakabidhiwa Rais kusubiri kupigiwa kura ya maoni mwaka 2016.
Habari kutoka bungeni zinadai kuwa wasiwasi wa
kutopatikana kwa theluthi mbili uko zaidi upande wa Zanzibar hasa baada
ya wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kususia Bunge
hilo.
Hofu nyingine inatokana na suala la Mahakama ya
Kadhi kutoingizwa, jambo ambalo limewagawa wajumbe huku kundi moja
likiapa kupiga kura ya hapana iwapo haitaingizwa.
Baadhi ya wajumbe wanataka Ibara ya 40 iingize
vifungu vinavyotamka kuwapo kwa mahakama hiyo ili uamuzi wake kuhusu
masuala ya ndoa, mirathi na talaka utambuliwe na sheria za nchi.
Hata hivyo, wajumbe wengine wanapinga suala hilo
wakitaka ibara hiyo ibaki kama ilivyo ili Serikali isijihusishe na
masuala ya uendeshaji wa jumuiya za dini.
Vilevile, Kifungu cha 22 (d) cha Rasimu kinachompa
mwanamke haki sawa na mwanamume kumiliki ardhi kinapingwa vikali na
baadhi ya wajumbe.
Pia baadhi ya wajumbe kutoka Zanzibar wanaona kuwa
pamoja na kwamba karibu asilimia 90 ya mambo waliyokuwa wakiyalilia
yameingizwa kwenye Katiba, bado Zanzibar haijapewa mamlaka kamili.
Hali hiyo imeifanya Kamati ya Uongozi chini ya
Sitta kufanya vikao vya mashauriano mfululizo baina yao na wajumbe wa
Kamati ya Uandishi ili kujaribu kuokoa jahazi.
Jana, vikao vya kamati 12 za Bunge ambavyo
vilikuwa vianze saa 8:00 mchana vililazimika kusogezwa mbele kusubiri
maelekezo kutoka Kamati ya Uongozi ambayo ilikuwa inakutana saa 9:00
alasiri.
Upigaji kura huo unafanyika chini ya kanuni mpya baada ya zile
za awali kufanyiwa marekebisho ili pamoja na mambo mengine, kuruhusu
wajumbe walioko nje kupiga kura kwa njia ya faksi na mtandao.
Katibu wa Bunge hilo, Yahya Khamis Hamad
alipotafutwa jana kufafanua maandalizi ya utekelezaji wa kanuni hiyo
inayokosolewa na makundi mbalimbali ya jamii, alisema kila kitu
kitafahamika leo.
“Sasa hivi ndiyo niko kwenye kikao na wenzangu
subirini kesho (leo) ratiba yote mtapewa,” alisema Katibu bila kutaka
kuendelea zaidi kujibu hoja za mwandishi wetu.
Septemba 22, mwaka huu, wajumbe wa Bunge hilo
walipitisha azimio la kuzifanyia marekebisho kanuni za 30,36 na 38 za
Bunge ili kurahisisha upigaji huo wa kura.
Chini ya marekebisho hayo, wajumbe watakaokuwa nje
ya Bunge kwa ruhusa ya maandishi ya mwenyekiti, wataruhusiwa kupiga
kura kwa njia ya faksi au mtandao.
Miongoni mwa kanuni zilizofanyiwa marekebisho ni
30 (1) ambayo sasa inasomeka kuwa akidi kwa kila kikao cha Bunge la
Katiba itakuwa ni nusu ya wajumbe hata kama ni kikao kwa ajili ya
uamuzi, ikimaanisha kwamba si lazima leo wawepo wajumbe wote, bali nusu
tu, ili upigaji kura uweze kufanyika.
Kanuni hiyo ndiyo iliongezwa fasili mpya ya 2A
kuruhusu wajumbe waliopo nje ya Bunge kwa ruhusa ya mwenyekiti,
wajumuishwe kwenye idadi ya wajumbe waliohudhuria kikao siku hiyo.
Kanuni nyingine iliyorekebishwa ni ya 36 kwa
kuongeza fasili mpya ya 1A ili kuruhusu mjumbe kuzipigia kura ibara zote
za sura moja au zaidi ya sura moja za Rasimu ya Katiba inayopendekezwa
badala ya kupigia sura mojamoja kama ilivyokuwa awali.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo mpya, endapo mjumbe
atapiga kura ya wazi basi atatamka ibara anazozikubali na asizozikubali
na anayepiga kura ya siri kuonyesha anazozikubali na anazozikataa.
Ili kukidhi kile kilichoelezwa na Katibu wa Bunge
kwamba Bunge Maalumu litatuma Ofisa wake Saudi Arabia kusimamia upigaji
kura kwa mahujaji, kanuni ya 38 ilirekebishwa.
Kanuni hiyo imeongezwa fasili mpya ya 1A na 1B ili
kumpa mamlaka Katibu wa Bunge kuwa msimamizi mkuu wa upigaji wa kura na
anaweza kumteua mtu yeyote kusimamia upigaji kura kwa niaba yake.
Baada ya kura zote za siri kupigwa, kura hizo
zitakusanywa na kupelekwa kwenye chumba maalumu kuhesabiwa mbele ya
mawakala walioteuliwa kwa ajili ya kusimamia kura hizo.
Mjumbe anayetaka kupiga kura ya wazi, ataitwa jina na Katibu au
mtu aliyeidhinishwa na katibu na atatamka kwa sauti maneno “Ndiyo” au
“Hapana” kuhusu Ibara husika au rasimu ya mwisho.
Mjumbe anayepiga kura ya siri au ya wazi nje ya
maeneo ya Bunge, ataelekezwa kwa maandishi na katibu baada ya
kushauriana na mwenyekiti kuhusu utaratibu.MWANANCHI
Post a Comment