DAR ES SALAAM.
MJADALA wa Mabadiliko ya Katiba jana ulihamia nje ya Bunge wakati Jaji Joseph Warioba alipomchambua mhadhiri maarufu nchini, Profesa Issa Shivji akimueleza kuwa si mkweli bali mpotoshaji wa Rasimu ya Katiba.
MJADALA wa Mabadiliko ya Katiba jana ulihamia nje ya Bunge wakati Jaji Joseph Warioba alipomchambua mhadhiri maarufu nchini, Profesa Issa Shivji akimueleza kuwa si mkweli bali mpotoshaji wa Rasimu ya Katiba.
Jaji Warioba, ambaye ni mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, pia amemtuhumu Profesa Shivji kuwa ndiye
mwanzilishi wa chokochoko za Zanzibar za kudai serikali tatu, jambo
ambalo sasa analigeuka kutokana na kuona hali imekuwa mbaya.
Kauli ya Warioba imekuja baada ya Profesa Shivji
kuichambua Rasimu ya Katiba jana asubuhi kwenye Kongamano la Vijana
lililoandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
lililokuwa na dhima ya Vijana Katika Kuimarisha na Kuendeleza Muungano
Baada ya Miaka 50. Tamasha hilo lilifanyika kwenye hoteli ya Blue Pearl,
Ubungo Plaza jijini Dar es salaam.
Akiwasilisha mada kwenye kongamano hilo, Profesa
Shivji alisema katika kujadili Muungano, wananchi hawana budi kuzingatia
mambo mawili ambayo ni nchi zinazozungumziwa kwenye Rasimu kuwa ni
Zanzibar, Tanganyika au Tanzania, ambayo alisema haina mamlaka katika
pande hizo mbili za Muungano.
Pia alisema suala la maadili kwa viongozi halina
budi kuangalia kuwa linazungumzia maadili ya viongozi wa Zanzibar,
Tanganyika au Tanzania na kwamba rasimu inazungumzia viongozi wa
Tanzania ambao hawana mamlaka kwa Tanganyika na Zanzibar.
Katika majumuisho yake, Profesa Shivji, ambaye
aliikosoa Rasimu kuwa haiwakilishi matakwa ya Watanzania kwa kuangalia
sampuli zilizotumika, alisema kwamba wajumbe wa Tume ya Jaji Warioba
walikuwa na nia njema.
Lakini Shivji akaenda mbali zaidi kwa kusema “the
road to hell is paved in good intention,” akimaanisha kuwa njia ya
kuzimu imetengenezwa kwa nia njema.
Akijibu hoja hizo, Jaji Warioba alisema Profesa
Shivji amegeuka maandishi yake yaliyokuwa yanachochea utaifa wa Zanzibar
na sasa anaona Tanganyika ndiyo hatari kwa Muungano.
“Shivji ni msomi na mimi najua anaelewa matumizi
ya takwimu,” alisema Jaji Warioba, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakati alipozungumza na gazeti hili
nyumbani kwake jana jioni.
“Nasema hapa, Shivji akiwa msomi, amekuwa intellectually dishonest (si mkweli kiusomi). Anapotosha kwa makusudi.”
Jaji warioba alisema Shivji ndiye amekuwa chanzo
cha uchochezi wa kitaifa Zanzibar kupitia maandishi yake. Alisema
waliokuwa wanadai serikali tatu kwa muda mrefu walikuwa wananchi wa
Zanzibar.
“Shivji alikuwa anasema Tanganyika imejificha
kwenye Muungano ili inufaike. Kwa hiyo anasema Tanganyika iwe wazi
isijifiche,” alisema Jaji Warioba.MWANANCHI
Post a Comment