Mjumbe
wa Bunge Maalumu la Katiba, Magdalena Sakaya (kushoto), akizozana na
Magdalena Likwina baada ya Semina ya Kupitia Vifungu vya Rasimu ya
Kanuni kuahirishwa kutokana na vurugu zilizotokea bungeni jana. Picha na
Silvan Kiwale
Ngumi mkononi ndilo neno jepesi ambalo linafaa kutumika baada ya vurugu kubwa kutokea jana ndani ya Ukumbi wa Bunge Maalumu la Katiba kiasi cha kumlazimisha Mwenyekiti wa Muda, Pandu Ameir Kificho kuahirisha semina kabla ya wakati wake.
Semina ya
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, imekuwa ikianza saa 4:00 asubuhi
hadi saa 7:00 mchana kabla ya kuendelea tena kuanzia saa 11:00 jioni
hadi saa 3:00 usiku. Jana, katika kipindi cha asubuhi, semina hiyo
iliahirishwa saa 6:17 licha ya kuanza saa tano asubuhi kabla ya kurejea
tena saa 10 jioni.
Ngumi
zilitaka kupigwa baada ya Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar,
Abubakari Hamis Bakari kuhoji uhalali wa Christopher Ole Sendeka na Ummy
Mwalimu kuchangia wakati hawakuwamo katika orodha ya wachangiaji jambo
ambalo liliibua mjadala mkali na kurushiana maneno kabla ya Mwenyekiti
Pandu Ameir Kificho kuahirisha semina hiyo.
Chanzo cha vurugu
Kificho
alimpa Ole Sendeka nafasi ya kuchangia Kifungu namba 58 cha rasimu ya
kanuni na baada ya kutoa mchango wake, Hamisi ambaye pia ni Mjumbe wa
Kamati ya Kanuni, alisimama na kumtaka Mwenyekiti Kificho kuacha
kuwateua watu ambao hawamo katika orodha ya wachangiaji.
Kificho
hakumsikiliza na badala yake, alimpa nafasi mjumbe mwingine wa Bunge
hilo Ummy Mwalimu ambaye pia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais,
kuchangia. Hata hivyo kabla hajafanya hivyo, Bakari alisimama tena na
kumzuia kuchangia kwa madai kuwa hakuwamo kwenye orodha ya wachangiaji.
“Mheshimiwa
Mwenyekiti, kama tutaendelea na utaratibu huu suala la kuchangia kanuni
linaweza kutupeleka hadi miezi sita bila ya kumaliza. Haya majina
hayakuwemo kwenye orodha ya wachangiaji na huyo aliyemaliza sasa Ole
Sendeka, naye hakuwamo, naomba tuache mchezo huu,” alisema Bakari.
Aliendelea:
“Sekretarieti inakuchomekea majina mwenyekiti na kama hivyo ndivyo,
basi tunatakiwa kuwachukulia hatua kali hawa kwani tunataka kujadili
hoja ambazo hazimo.”
Bakari
alisema wajumbe waliotakiwa kuchangia ni wale ambao walipeleka majina
kwa makatibu wa Bunge hilo pamoja na michango yao kwa maandishi ili
wapewe nafasi ya kuzungumza, lakini Kificho alikuwa akiwateua wajumbe
ambao hawamo katika orodha hiyo.
Kificho ajibu
“Mimi
sina tatizo na jambo hilo, mkisema tuendelee basi sawa, lakini mkitaka
tufanye mambo kwa uzuri inawezekana pia, jambo la muhimu ni kuwa tupo
hapa kutengeneza Katiba ya wananchi siyo ya vyama.”
Kelele zilianza kusikika huku wajumbe
wakiimba kuwa mwenyekiti anayumba… na kumtaka mwenyekiti atoke nje na
kukiacha kiti, kwani anafanya upendeleo.chanzo Mwanainchi
Post a Comment