Waziri
wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwinyi na Makamu wa Rais, Dk
Gharib Bilal, katika Mkutano wa mwaka wa Uzazi wa Mpango, Oktoba mwaka
huu. Katika Mkutano huo Tanzania ilionekana bado ina matumizi ya chini
ya dawa za uzazi wa mpango. Picha na Maktaba.
Pamoja na
kuwa ni njia nzuri ya kuzuia ujauzito, vidonge vya Uzazi wa Mpango
vinatajwa kusababisha ugonjwa wa macho ujulikanao kama Glaucoma, unaoelezwa kuwa ni chanzo kikuu cha upofu.
Ugonjwa huu unaelezwa kuwa sababu kubwa ya kusababisha upofu kwa wanawake wanaotumia vidonge hivi kwa muda mrefu.
Hayo yamebainishwa kwenye Utafiti wa Afya na Lishe uliofanywa na Kituo cha Udhibiti na Uzuiaji wa Magonjwa cha Marekani(CDCP).
Utafiti huo unasema kuwa, seli zilizoko katika neva za macho zina homoni za estrogen ambazo hufanya kazi ya kulinda macho, vidonge hivyo huingilia mchakato huo wa ulinzi kwa kupunguza kiwango cha homoni hizo.
Unasema
kuwa wanawake wanaofunga hedhi mapema au wanaotumia vidonge ambavyo
huzuia kuzalishwa kwa vichocheo vya estrogen, na dawa za saratani ya
matiti, huweza kupata upofu.
Wanawake
zaidi ya 3,400 wenye umri wa zaidi ya miaka 40 walifuatiliwa kwa zaidi
ya miaka mitano ikiwa ni sehemu ya utafiti huo.
Profesa
Shan Lin wa Chuo Kikuu cha Carlifonia, San Francisco anasema wanawake
wanaotumia vidonge hivyo kwa zaidi ya miaka mitatu, wanatakiwa kupima
maradhi ya macho aina ya Glaucoma na afya zao zifuatiliwe kwa uangalifu
na wataalamu wa macho.
Utafiti
huo umebaini kuwa wanawake waliotumia vidonge hivyo kwa miaka zaidi ya
mitatu walikuwa na hatari kwa asilimia tano ya kupata upofu usababishwao
na glaucoma ukilinganisha na wasiotumia vidonge hivyo.
Kiongozi
wa utafiti huo, Dk Louis Pasquale wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Havard
anasema vichocheo vya Estrogen vina umuhimu katika seli za retina
ambazo zinajulikana kwa kupokea homoni hizo.
“Kuwepo
kwa homoni za estrogen kunazisaidia seli hizo kuwa hai kwa hiyo wanawake
wanapotumia vidonge vya uzazi, homoni hizo huharibiwa na kurahisisha
uharibifu wa macho,” anasema Dk Pasquale.
Daktari
Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Dk Cyriel Masawe wa Chuo Kikuu cha Tiba
cha Muhimbili (MNH) anasema ni hatari kwa wasichana wadogo ambao
hawajaolewa kutumia dawa hizo ovyo.
“Kwa
mfano mikoa ya Lindi na Mtwara, tumegundua wasichana wadogo ambao
hawajaolewa wanatumia zaidi sindano za uzazi wa mpango na vidonge,”
anasema Dk Masawe
anasema si vyema watu kuzitumia dawa za Uzazi wa Mpango kwa mazoea na
endapo wataona ni vyema kufanya hivyo, washauriane na wataalamu wa afya.
Anasema
kuwa elimu inahitajika kwa kina kuhusu matumizi ya dawa hizo kwani wapo
baadhi ya watu wanaozitumia bila mpangilio wala utaratibu maalum.
“Hizi dawa zinasaidia lakini zisipotumiwa kwa uangalifu, huenda zikasababisha madhara,” anasema Dk Masawe.
Kwa
upande wa utafiti huo uliojikita kuangalia madhara ya vidonge hivyo kwa
wanawake, watu wanaovitumia wanatakiwa kuwa makini na uhusiano uliopo
kati ya afya ya uzazi na maradhi ya macho hasa kama mtumiaji amefunga
hedhi mapema.
Matokeo
ya utafiti huo yaliyotolewa katika mkutano wa kila mwaka wa Chuo Kikuu
cha Mfumo wa Macho Marekani (USP), yanasema wanawake zaidi ya 3,046
walifanyiwa uchunguzi kuhusu afya ya uzazi na maradhi ya macho.
Pamoja
na sababu nyingine za maradhi ya macho, wanasayansi waliofanya utafiti
huo wanasema kutumia vidonge vya uzazi kwa muda mrefu, ndicho chanzo
kikuu cha upofu na kutaja sababu nyingine kuwa ni historia ya familia,
shinikizo la ya macho na kisukari.
Watalaamu wa afya nchini wanasema bado madhara ya dawa hizo yanatofautiana kulingana na aina ya dawa anayotumia mhusika.
Madhara
mengine ya dawa hizi ni pamoja na kichefuchefu, kichwa kuuma, matiti
kuuma, kuongezeka uzito na kupata hedhi bila mpangilio.
Dk Joseph
Matiku wa Kituo cha Afya, Mugumu, Serengeti anasema, hatari zaidi ni
kwa binti wanaotumia dawa hizo kwa muda mrefu kabla hawajaanza maisha ya
ndoa.
“Wapo
wanawake ambao wanapata uvimbe kwenye kizazi kutokana na matumizi ya
muda mrefu ya dawa hizi. Ingawa hakuna utafiti uliofanyika kuthibitisha
hili, lakini wanawake wengi wanaotumia dawa hizi hapa nchini wanapata
uvimbe maarufu wa Fibroids” anasema.
Hata
hivyo, Oktoba mwaka huu, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein
Mwinyi anasema Wizara ya Afya ipo kwenye harakati za kutafuta fedha ili
kuhakikisha asilimia 60 ya wanawake wanaostahili kupanga uzazi wanapata
dawa husika.
Mwaka
jana wakati wa Mkutano wa Uzazi wa Mpango uliofanyika London Uingereza,
Rais Jakaya Kikwete aliahidi kuwa hadi kufikia mwaka 2015 Tanzania
itafikisha asilimia 60 katika huduma za uzazi wa mpango.Vilevile
katika Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Uzazi wa Mpango uliofanyika Oktoba
mwaka huu, Makamu wa Rais Dk Gharib Bilal alisema juhudi za ziada
zinahitajika kuhakikisha kiwango cha watumiaji wa huduma za uzazi wa
mpango, kinaongezeka ili kutimiza lengo la kimataifa ya kuongeza idadi
ya watumiaji wa huduma hiyo.
Takwimu
za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa, kiwango cha matumizi
ya huduma za uzazi wa mpango kwa nchi zilizoendelea ni asilimia 72,
huku Tanzania iliyo kwenye kundi ya nchi zinazoendelea ikiwa ni asilimia
27 tu.
Dawa za uzazi wa mpango hufanyaje kazi?
Vidonge vya uzazi wa mpango hufanya kazi ya kuweka uwiano katika kiwango cha vichocheo.
Katika hili, kazi kubwa ni kuzuia homoni za estrogen kuongezeka na kufikia kiwango cha kati au cha juu.
Bila
homoni ya estrogen, tezi ya pituitari haiwezi kuifanya mirija ya uzazi
kuruhusu mayai yaliyochavushwa kwenda kukutana na mbegu za kiume kwa
ajili ya utungishwaji wa mimba.MAGANGAONE
|
Post a Comment