0
Wakati nasoma historia ya watu mbalimbali waliofanikiwa duniani na walioweza kutengeneza fedha na utajiri mkubwa kutokana na kufuata na kuishi ndoto zao, nilishangaa sana kuona ni jinsi gani watu hawa walikopitia hadi kuweza kufanikiwa pamoja na mazingira magumu yaliyo wazunguka ila hawakuruhusu mazingira hayo kuwa kikwazo kwao cha kufanikisha ndoto walizokuwanazo. Ukifatilia historia za watu hawa unaweza ukajifunza kitu kikubwa sana ambacho kinaweza kukufanya na wewe uone wepesi wa kufanikiwa katika maisha yako na hatimaye kuona uhalisia wa kutimiza ndoto yako.
Baadhi ya watu hawa wachache wafuatao wanaweza kukushangaza sana utakaposoma historia ya mahali walipoanzia hasa katika mazingira waliyotokea na kuweza kufanikisha ndoto zao pamoja na mazingira yao kuwa magumu sana kwao, lakini cha ajabu hawakuzuiwa na mazingira hayo hadi walipoona wamefanikisha ndoto zao. Hawa ni wajasiriamali wakubwa duniani waliowahi kuishi na wengine wanaoishi hadi hivi leo.
1: Henry Ford alianzisha kampuni yake ya Ford Motor Company akiwa ndani ya gereji yake. Leo hii kampuni ya Ford ni mojawapo ya kampuni inayozalisha magari mazuri na ya thamani kubwa duniani ingawa Ford mwenyewe alishafariki ila anakumbukwa kwa ushujaa wake. Hii ni pamoja na Ford kupitia mazingira magumu kimaisha hata kuwahi kufanya kazi chini ya Thomas Edison mwanzilishi wa kampuni wa General Electric na badae kuweza kuanzisha kampuni yake ya Ford Motor.
2: Michael Dell alianzisha Dell Computers akiwa ndani ya Bweni la chuo chake (college dorm room). Leo hii kampuni ya Dell ni miongoni mwa kampuni kubwa duniani inayojishughulisha na utengenezaji wa kompyuta na vifaa vingine mbalimbali vya kieletroniki kama vile kamera, printa, nakadhalika.
3: Steve Jobs alianzisha kampuni yake ya Apple akiwa ndani ya gereji baada ya kupitia mazingira magumu. Leo hii naamini hakuna mtu hasiyefahamu kampuni ya apple kama mojawapo ya kampuni inayozalisha bidhaa za kieletroniki zilizo bora zaidi na za thamani kubwa kuliko kampuni nyingine yoyote ile duniani. Bidhaa kama vile simu janja za Iphone, kompyuta za Apple Mac, Saa, Tv, tablet, nakadhalika. Leo hii Jobs naweza kumfananisha na mtu aliyekufa ingawa anaishi, hii ni kutokana na kutimiza ndoto yake kubwa ambayo dunia nzima inanufaika nayo.
Steve Jobs 1
4: Sergey Brin na Larry Page waliweza kuanzisha kampuni ya Google wakiwa chuoni. Hapo ulipo naamini unafahamu kabisa haiwezi kupita siku kama unatumia kifaa cha inteneti husiweze kutumia Google kwa ajili ya kuweza kupata taarifa mbalimbali unazozitaka mtandaoni. Hii ni kutokana na watu wawili ambao hawakuangalia mazingira yaliyowazunguka wakiwa chuoni wakatumia fursa ya muda wao walioupata kugundua mtandao wa Google na leo hii umekuwa na faida kwa watumiaji maelfu na elfu wa mtandao wa inteneti.
5: Mark Zuckerberg ambaye ni mwanzilishi na mmiliki wa Facebook. Mark aliweza kuanzisha facebook miaka 12 iliyopita tangu hapo February 4, 2004 akiwa katika chuo kikuu cha Harvard pamoja na wenzake ambao ni Eduardo Saverin, Andrew McCollum, Dustin Moskovitz, and Chris Hughes. Hii ni wazi kuwa mazingira ya chuo hayakuwa kikwazo na sababu kubwa kwa Mark kuitimiza ndoto yake aliyokuwa nayo. Jiulize wewe ni mwanafunzi ukiwa upo chuo muda huu au mahali popote pale, ni ndoto gani uliyonayo muda huu ambayo una hofu ya kuitimiza hadi sasa kutokana na mazingira ya shule uliyonayo? Tumia unachosomea kuwa sababu ya kufikia ndoto yako, na si elimu unayopata kuwa kikwazo cha kufika mahali unapotaka.
6: Hewlett na Packard ni waanzilishi na wamiliki wa kampuni ya HP ambao kwa majina yao halisi ni William “Bill” Redington Hewlett na David “Dave” Packard. Hawa ndio watu wawili walioanzisha kampuni ya teknolojia ya HP inayotengeneza kompyuta na programu (software) mbalimbali za kompyuta. Walianzisha kampuni yao kwa mara ya kwanza wakiwa ndani ya gereji.
7: Bill Gates ambaye ndio tajiri wa kwanza duniani hadi hivi sasa anayejishughulisha na kuuza programu za kompyuta zilizo katika mfumo wa programu zake anazotengeneza mwenyewe za Microsoft. Bill Gates anauza programu (software) zake katika kampuni ndogo ndogo zinazojishughulisha na mambo ya kompyuta, nakadhalika. Aliwahi kukataliwa mara nyingi kabla ya kufanikiwa kama anavyoonekana hivi leo, na zaidi sana leo hii ndiye tajiri wa kwanza duniani kwa mujibu wa orodha ya jarida la Forbes. Leo hii kompyuta nyingi duniani zinatumia mfumo na programu za Microsoft hii ni kwa sababu ya mtu aliyekataliwa kutokana na ndoto yake aliyokuwa nayo lakini hakukata tamaa hadi akafanikisha ndoto aliyokuwa nayo.
Hao wote na wengine wengi sana ambao sitoweza kuwaandika wote mahali hapa, ni sehemu tosha ya funzo kwangu na kwako pia hasa juu ya kuzifuata na kuzifanikisha ndoto zetu tulizonazo. Nikuulize swali, Ni ndoto gani uliyonayo leo hii ambayo umekuwa ni mgumu kuifanikisha kutokana na mazingira uliyonayo au yaliyokuzunguka muda huu?
Nataka nikuambie mazingira yaliyokuzunguka ni muhimu sana kwa ajili ya kufanikisha ndoto yako uliyonayo muda huu, haijalishi mazingira hayo yapo namna gani na ndio maana Mungu akakuweka katika mazingira hayo ili uweze kutengeneza ushuhuda na kuwa msaada na faraja kwa wengi. Usitegemee mazingira yoyote mengine unayoweza kuyapata ili uweze kuanza kuchukua hatua juu ya ndoto yako. Mazingira uliyonayo muda huu hapo ulipo ndio yanayoamua hatima njema ya ndoto yako, haijalishi upo chuoni kama Mark Zuckerberg au upo mazingira ya gereji kama Steve Jobs na Henry Ford, au upo mahali popote pale kwenye mazingira unayoona ni magumu kwako iwe ni kijijini hakuna umeme, nakadhalika. Nataka kukuambia mazingira hayo hayo uliyonayo muda huu ndio yatakayoamua hatima njema ya mafanikio ya ndoto yako.
Anza leo kutimiza ndoto yako pasipo kuzuiliwa na lolote ili uweze kuona matunda makubwa juu ya maisha yako. Hebu jiulize kama Michael Dell angeamua kuangalia mazingira aliyokuwa nayo leo hii tungepata wapi kutumia kompyuta zake za Dell. Kama Mark Zuckerberg angeamua kuangalia mazingira ya chuo aliyonayo leo hii tungepata wapi kuwasiliana na kujuana kama tulivyo hivi sasa na kusaidiana kupitia mtandao wa facebook. Nataka kukuambia unapopoteza fursa ya kufanya kitu kizuri ulichonacho kutokana na kuangalia mazingira ya mahali ulipo, basi unakuwa unapoteza nafasi kubwa ya kusaidia wengine na zaidi sana na wewe kupiga hatua kubwa kwenda mbele  unayotakiwa kufika kwenye muda huu ulionao.
Amini katika uwezo ulionao na chukua hatua katika hayo mazingira uliyonayo na hakika utaona mafanikio yako yakitokea mapema zaidi.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHI NDOTO YAKO.

Post a Comment

 
Top