0


MBUNGE wa Mtera, Livingstone Lusinde amelaani tukio la mauaji ya kinyama ya watafiti wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Selian (SARI) cha Arusha, yaliyotokea katika Kijiji cha Iringa Mvumi kwa kuchomwa moto mapema mwezi huu.

Mbunge huyo amewataka wananchi waliokimbia kurudi kwenye makazi yao na kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ili wote waliohusika katika tukio hilo wakamatwe.

Lusinde, ambaye ni Mbunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyasema hayo jana, alipokuwa akifafanua kuhusu taarifa zilizoandikwa na gazeti hili, zikimhusisha na tuhuma za kuchochea wananchi na kubainisha kuwa tuhuma hizo zinaweza kuwa njama za maadui zake za kutaka kumchafua kisiasa.

“Sijawahi kuhojiwa kuhusu uchochezi. Taarifa hizo si za kweli na zimeniletea usumbufu mkubwa,” alisema Lusinde.“Bado naendelea kulaani tukio lile baya la kumwaga damu za wananchi wasio na hatia, wananchi waache kuji chukulia sheria mikononi. “Nimesikitishwa na taarifa kuwa nilihojiwa na polisi juu ya tukio la kuuawa kwa watafiti, jambo ambalo si kweli. Tangu niwe kiongozi sijawahi kuchochea wananchi kwa jambo lolote,” alieleza Lusinde na kuongeza: “Mimi nina maadui wengi, hilo siwezi kubisha, adui anaweza kutumia watu ili wanichafue, lakini hilo si sawa kwenye maadili ya uandishi wa habari.”

Alisema amekuwa mbunge katika Jimbo la Mtera kwa kipindi cha pili sasa na hakuwahi kushuhudia watu wakifanya matukio ya kinyama, kama lililotokea Iringa Mvumi.

“Siku ya tukio sikuwa kijijini Iringa Mvumi, nilikuwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu na tangu uchaguzi umepita sijawahi kufanya mkutano wowote kwenye kile kijiji,” alifafanua.

Alisema amekuwa akifanya kazi kwa kushirikiana na madiwani na wenyeviti wa vijiji. Lusinde alifafanua kwamba alikwenda Kituo cha Polisi kwa ajili ya kuwasalimia viongozi na wananchi, ambao wako mahabusu kuhusu tukio lile akiwemo Diwani Robert Chipole, Mwenyekiti wa Kijiji Albert Chimanga na mwananchi mmoja aitwaye Noco Kwanga.

“Niliwasalimia na kuwauliza hali ilivyokuwa wakasema hawakuhusika na nikawataka watoe ushirikiano kwa vyombo vya dola ili haki iweze kutendeka na bado polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo,” alisema na kukiri kuwa mauaji hayo yamesababisha wananchi wakimbie na shughuli zote zimesimama.

Alisema kwa mujibu wa taarifa alizopata jana kwa Katibu wake, Patrick Nyambuya ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Makang’wa, hali katika kijiji kile inaanza kurudi polepole kuwa ya kawaida. “Wananchi wameanza kurudi kwenye nyumba zao na maisha yanaanza kurejea kwenye kijiji hicho,” alisema.

Alisema sasa wananchi ambao ni raia wema, wameanza kuona gharama ya kupoteza amani na waone hilo ni fundisho kwa wananchi wa jimbo zima la Mtera.

“Nasisitiza wananchi kurudi na kuwatambua wahusika waliotekeleza tukio lile,” alisisitiza Lusinde, mmoja wa wabunge maarufu kwa kujenga hoja bungeni.

Alisema kabla ya tukio la mauaji ya watafiti, kulikuwa na tukio lingine la mauaji ya mwanamke aliyejulikana kwa jina la Tatu, mkazi wa Mvumi Misheni, ambaye alikutwa ameuawa shambani eneo la Iringa Mvumi.

“Naamini vyombo vya dola vinafanya kazi yake katika kuwatafuta na kuwakamata wauaji na kama kuna mwananchi ana taarifa za mauaji ya Tatu asisite,” alisema na kuongeza kuwa pia ushirikiano na viongozi wa vijiji ni mzuri na mchango wa serikali ni mkubwa katika kutekeleza shughuli za maendeleo.

Watu watatu kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Serian (SARI) Arusha, ambao ni Nicas Magazine aliyekuwa dereva pamoja na watafiti wawili, Teddy Lumanga na Jafari Mafuru waliuawa kwa kucharangawa kwa mapanga na kisha kuchomwa moto na watu wanaoaminika kuwa wakazi wa Iringa Mvumi, Oktoba mosi, mwaka huu walipokuwa wamekwenda kijijini humo kufanya utafiti wa masuala ya udongo.

Post a Comment

 
Top