Pamoja akiwa mwenye umri mdogo wa miaka 8, Hugh Herr alikuwa mwenye
shauku na ndoto kubwa ya kuwa mkwea milima (Rock Climber), na aliweza
kufanya hivyo kwa wakati huo baada ya kuanza kupanda mlima uliopo nchini
canada wenye urefu unaofikia 3,544 (11,67ft) unaojulikana kwa jina la
Mount Temple. Alipofikia umri wa miaka 17 ikiwa ni mwezi januari 1982
Herr aliendelea kupigania kufanikisha ndoto yake kwa kupanda mlima
mwingine uitwao Mount Washington uliopo mji wa New Hampshire nchini
mwake Marekani.
Kwa wakati huu akiwa na rafiki yake wa karibu Jeff Blatzer aliyekuwa
na umri wa miaka 20 waliweza kuanza safari yao ya kuamua kupanda mlima
Washington, huku kukiwa ni kipindi cha baridi na barafu kali iliyokuwa
kwenye kiwango cha -29 C. Hali hii kwao haikuwa kikwazo cha kuwazuia
kutimiza ndoto yao waliyokuwa nayo kwa muda mrefu tangu hapo awali. Muda
mchache baada ya kupanda mlima ule wakiwa katika kutimiza ndoto yao
ghafla wakaanza kuteseka kutokana na hali ile ya baridi na barafu kali
iliyowazidi na ikawa ni changamoto kubwa kwao kuendelea kukwea katika
mlima ule; ndipo wote wawili walipochoka wakaamua wajiachie na kuangukia
katika bonde lililokuwa chini yao.
“Commitment leads to action. Action brings your dream closer.”
-Marcia Wieder
Baada ya tukio hilo la kuanguka kwa Herr na rafiki yake, kwa pamoja
walijikuta kwenye hali ngumu baada ya kuchukua muda wa siku 4 kabla ya
kuokolewa wakiwa katika hali ya kuzidiwa na baridi kali iliyofanya
watengeneze pango dogo kwa kupitia barafu na kuamua kukumbatina pamoja
ili kuamsha hali ya joto la kuwasaidia dhidi ya hali ile ya baridi.
Walipofanikiwa kuokolewa na baada ya miezi miwili kupita ikiwa ni mwezi
March, Herr alijikuta akipoteza miguu yake yote miwili baada ya
madaktari kugundua haiwezekani kupona kutokana na kuumia sana na kuamua
kuikata kutokana na ajali aliyoipata. Lakini kwa upande wa rafiki yake
ambaye ni Jeff, yeye alijikuta akipoteza vidole vya mguu wa kushoto na
mkono wa kulia.
Hapo ndipo Herr alijikuta akipewa agizo kutoka kwa madaktari zake la
kuacha mara moja suala la kukwea milima baada ya kupoteza miguu yake
yote miwili, lakini jambo hilo lilikuwa gumu kwa Herr kuacha kufanya kwa
kuwa ndani yake alipenda kuwa mkwea milima atakayeweka rekodi katika
taifa lake. Na ndivyo ilivyokuwa na alifanikiwa katika hilo, kwani leo
hii Herr anatajwa kama mtu bora zaidi (the best) aliyeweza kukwea milima
katika kipindi kigumu ikiwa hadi leo hii pamoja na kutokuwa na miguu
yake yote miwili.
Ninaweza kusema mambo mengi kuhusu mtu huyu ambaye hadi sasa kwa
mahali alipofikia ni pakubwa sana, ila kwa machache haya tunaweza
kujifunza jambo kubwa sana kwetu. Kwa sasa pia Herr ni mmiliki wa
kampuni ya kiteknolojia (Center For Extreme Bionics) inahusika na
kutengeneza vifaa vya bandia vya kuwekeza kwenye miili ya watu
waliopoteza viungo vyao vya asili kama vile mikono, miguu, nakadhalika,
akijulikana kama Dr. Hugh Herr, hii ni baada ya kufanikiwa kujiendeleza
katika chuo kikuu cha Harvad nchini Marekani.
Unaweza kufikiri binafsi juu ya mtu huyu jinsi gani alivyokuwa na
shauku kubwa juu ya kutimiza ndoto yake? Mara nyingi sana ni ngumu kwa
watu wengi kufikia hatua ya kiwango cha juu cha kujitoa ili kutimiza
ndoto zetu. Herr hakuweza kukata tamaa hata baada ya kupoteza miguu
yake, na unaona wazi kabisa hakupoteza miguu yake kwa ajili ya jambo
lingine lolote bali ni kwa ajili ya safari ya kutimiza ndoto yake
aliyokuwa nayo muda mrefu, na pamoja na kupoteza miguu yake hiyo
haikumfanya arudi nyuma na kuacha kuifuata ndoto yake kwa mara nyingine.
Alikuwa radhi kufanya vizuri zaidi pamoja hakuwa na miguu yake halisi
akitumia miguu ya bandia (prosthetic legs), na aliweza kufanya vyema
zaidi kuliko mwanzo alivyokuwa na miguu yake.
Kuna sababu nyingi sana nyuma ya mtu yoyote anayetaka kukata tamaa
kwenye jambo fulani. Unaweza kukata tamaa kwenye mahusiano, kwenye
elimu, kwenye kazi au biashara unayoifanya; fahamu kuna kitu
kinachotupelekea kukata tamaa binafsi. Nakushauri ni vyema ufahamu ni
nini kinachotaka kukupelekea kukata tamaa kwenye ndoto yako, usikubali
kukata tamaa haraka kwa sababu ya kushindwa mara moja juu ya jambo
fulani bali unahitaji kupambana hadi mwisho ili kuhakikisha unafikia
ndoto yako. Kumbuka wakati umelala usiku kwa amani na furaha kwenye
kitandani chako, kuna wengine wanazurura mitaani wakiwa hawana mahali pa
kwenda na kulala kama wewe. Lakini watu hawa hawakati tamaa kwenye
maisha yao na wanazidi kusonga mbele kila kukicha. Ni vigumu sana kwetu
kufikiri watu hawa wana uwezo gani wa kupambana na maisha yao kila
panapokucha pasipo kukata tamaa.
Kuna kipindi fulani unapokuwa na shauku na ndoto fulani unayotaka
ifanikiwe katika maisha yako, itakubidi ujitoe kikamilifu pasipo
kuangalia gharama ya aina yoyote iliyopo mbele yako inayotaka kukuzuia
kufanya hivyo, ilimradi kuhakikisha unatimiza na kuifikia ndoto yako
uliyonayo. Nakusihi usitazame mazingira ya aina yoyote ile
yanayokuzunguka bali amua kuweka msimamo wa kusonga mbele ili uweze
kuhakikisha unafikia ndoto yako na kufanikiwa katika maisha yako.
Haijalishi ni hatari gani inayojitokeza mbele yako kukuzuia kutimiza
ndoto yako, songa mbele hadi uone matokeo makubwa kwenye hiyo ndoto ili
uweze kubadili maisha yako kuwa kwenye viwango (level) nyingine.
Usijaribu kujihurumia dhidi ya vikwazo vinavyojitokeza mbele yako hata
kuacha kutimiza ndoto yako uliyonayo, kujihurumia ni kuamua kupoteza
nafasi ya ushindi maishani mwako.
“Does anyone think that victory is possible without facing danger?”
-Franklin D. Roosevelt
Jiulize ni nini ndoto ya maisha yangu? Je, umekata tamaa kufuata na
kuishi ndoto yako? Ni jambo gani linalokuzuia muda huu kuitimiza ndoto
uliyonayo? Kama Herr hakukata tamaa kuifata ndoto yake hadi kufikia
kupoteza miguu, ni kwa nini wewe uwe miongoni mwa watu wanaokata tamaa
muda huu mapema kwa ajili ya kutimiza ndoto waliyonayo. Nakusihi inuka
na amua kutimiza ndoto yako kwa faida yako na ya kizazi chako hapo
badae.
Kila unapotaka kukata tamaa, jiulize ni kwa nini unataka kukata
tamaa? (Why you give up?) Kisha mkumbuke Hugh Herr. Kumbuka ni wewe
unayetakiwa kupambana kwa ajili ya kuhakikisha unatimiza ndoto yako,
matarajio yako, malengo na mipango uliyonayo, nakadhalika. Kama ukikata
tamaa leo, amini kabisa hutoweza kufikia mahali popote unapotaka kufika
katika maisha yako.
JIAMINI NA AMINI UNAWEZA. ISHINDOTOYAKO.
Be Unstoppable! Don’t Stop. Never Give Up On Your Dream.
Post a Comment